Ili kuhakikisha wanatengeneza nidhamu kwenye timu, uongozi wa Simba umeliagiza Benchi la Ufundi la timu hiyo kumuandikia barua ya onyo kali mshambuliaji wake Mganda, Hamis Kiiza.
Hatua hiyo imekuja siku chache tangu uongozi wa Simba utangaze kumsimamisha beki na nahodha wake msaidizi, Hassani Isihaka kwa kile kilichodaiwa kuonyesha utovu wa nidhamu kwa kocha wao Mganda, Jackson Mayanja.
Mara ilivyotangazwa kusimamishwa kwa Isihaka, Kiiza alimtetea beki wake huyo katika Mtandao wa Kijamii wa Instagram kitendo ambacho kinadaiwa kuwa kiliwakasirisha viongozi wa Simba.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa tayari wamemuagiza meneja wa timu hiyo, Abbas Ally kumuandikia barua ya onyo mshambuliaji huyo.
Taarifa kutoka ndani ya kambi ya Simba iliyopo Morogoro imeeleza kuwa Kiiza aliomba radhi kwa alichokifanya kwa kuwa kilionekana kama anaukosoa uongozi.
Aidha, jana, Kiiza aliutumia ukurasa wake wa Instagram kujitetea kuwa hakuwa na lengo baya kwa kuwa nia yake ilikuwa kufafanua kuwa Isihaka hana kawaida ya kuwa mtovu wa nidhamu bali kuna watu wamekuza mambo hasa magazeti na siyo viongozi wake.
0 COMMENTS:
Post a Comment