March 21, 2016


Siri ya Simba kufanya vizuri mfululizo katika mechi zake za Ligi Kuu Bara hivi karibuni imefichuka baada ya ushindi wa juzi Jumamosi ilioupata mkoani Tanga ilipopambana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani. 

Siri hiyo si nyingine bali ni uamuzi wa uongozi wa Simba kupitia kwa rais wake, Evans Aveva ulioufanya hivi karibuni baada ya kuamua kumteua aliyewahi kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Mzee Hassan Dalali kuwa mshauri mkuu wa benchi la ufundi la timu hiyo.

Dalali alikabidhiwa jukumu hilo kwa siri na uongozi huo baada ya mwenendo mbaya wa timu hiyo katika mechi zake za awali za ligi kuu.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa, tangu Dalali alipokabidhiwa timu hiyo, imeshinda zaidi ya mechi 12 na imepoteza moja tu dhidi ya Yanga ambapo ilifungwa kwa mabao 2-0.

“Hali hiyo imewafanya viongozi wetu kuwa na matumaini makubwa kuwa safari hii tunaweza kuwa mabingwa wa ligi kuu kwa sababu Dalali amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kulituliza benchi letu la ufundi lakini pia viongozi kutomwingilia kocha katika kazi yake.

“Ukiachana na hilo pia Dalali anaijua vizuri ligi kuu kwani katika kipindi chake Simba ilikuwa ikifanya vizuri, hivyo atatusaidia kukabiliana na ujanjaujanja wote ambao umekuwa ukifanywa kwa ajili ya kuimaliza timu yetu,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Dalali alisema: “Ni kweli kabisa hivi sasa nimekabidhiwa timu na uongozi na ninavyoongea na wewe mida hii nipo katika basi na timu tunatoka Tanga.


“Tangu nikabidhiwe jukumu hilo ni muda mrefu kidogo kama mechi kumi na kitu hivi zilizopita, hata hivyo kuhusiana na mambo mengine yanayohusu timu sasa siwezi kuyazungumzia, naomba unisamehe kwa hilo.” 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic