March 26, 2016


Straika Amissi Tambwe amesema haina haja ya mashabiki wa Yanga kuihofia Al Ahly kwani wana uwezo na wamepania kuifunga timu hiyo ya Misri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Yanga itaikaribisha Al Ahly katika mchezo wa kwanza wa 16 Bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika nchini wikiendi ya Aprili 9, mwaka huu.

Tambwe raia wa Burundi amesema kutoka kwao Burundi kwamba, Wanayanga wanatakiwa kutokuwa na wasiwasi juu ya mechi hiyo kwani anaamini kabisa wanauwezo wa kuitupa nje Al Ahly.

Alisema kwa upande wake ana uchu mkubwa wa kuhakikisha Yanga inafanya vizuri katika mechi zote mbili ambazo itacheza na Al Ahly timu maarufu Afrika.

“Al Ahly ni timu nzuri kila mtu analijua hilo lakini hata sisi Yanga tuna timu nzuri pia na tunao uwezo mkubwa wa kuiondoa kwenye michuano hiyo kama tulivyofanya kwa APR.

“Nawaomba Wanayanga wasiwe na hofu juu ya hilo kwani binafsi nimejipanga na ninaendelea kujiweka fiti kwa ajili ya mechi hiyo hivyo Mungu akipenda kila kitu kinawezekana,” alisema Tambwe.


Tambwe mwenye mabao 17 katika Ligi Kuu Bara na moja kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, yupo Burundi akiitumikia timu yake ya taifa ambayo Jumatatu ijayo itacheza na Namibia katika kufuzu Kombe la Afrika 2017.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV