March 26, 2016


Na Saleh Ally
BAADA ya kujua timu ya wakongwe ya Barcelona inakuja nchini Aprili, mwaka jana, niliamua kuahirisha safari moja ili niwaone.

Pamoja na kuwa nilitaka kukutana na wachezaji kadhaa wakongwe kwa sababu nilizokuwa nazo, lakini nilitamani zaidi kuzungumza na Hendrik Johannes Cruijff maarufu sana kama Johan Cruyff.

Nilitamani kuzungumza na Cruyff kuhusiana na ishu ya La Masia, kituo cha kukuzia vipaji cha Barcelona ambacho mawazo yake yalikifanya kiwe bora.

Nilijua mengi kuhusu gwiji huyo kwa kusoma zaidi lakini kocha wa zamani wa Yanga, Ernie Brandts ndiye aliyenishawishi kumpenda zaidi baada ya kuniambia pamoja na Uholanzi kuwa na vipaji lundo vya soka, haijawahi kupata mchezaji mfano wa Cruyff.

Unapokutana na Cruyff, unakuwa umekutana na mtu kariba ya Lionel Messi au Cristiano Ronaldo. Kweli hana mtu wa kufananishwa naye Uholanzi, England hata Hispania.

Hakika ana rekodi kibao na huenda utachoka hata kuzitaja zote. Mfano, alifunga mabao 405 katika muda wote aliocheza, akiwa Ajax kama mchezaji na kocha aliwapa makombe ya ubingwa ukiwepo wa Uholanzi.

Ajax alicheza misimu mitatu, Barcelona misimu minane na akawapa ubingwa Hispania akiwa mchezaji na akiwa kocha. Amekuwa mchezaji bora wa Uholanzi mara tatu pia.
Amekuwa mwanasoka wa dunia (Ballon d’Or) mara tatu. Anayeshikilia nafasi hiyo kwa sasa na anapambana kumpita ni Ronaldo.

Pamoja na yote haya, nilichotaka kujua zile sifa za La Masia pia Total Football ambao ndiyo wakati mpira ulitoka katika “uzamani” na kwenda maisha ya kisasa.
Kumbuka Cruyff ni mkongwe hasa, wachezaji wake leo ndiyo wakongwe na maarufu kama makocha Pep Guardiola (Bayern Munich), Ronald Koeman (Southampton) na wachezaji nyota kama akina Romario, Hristo Stoichkov, Michael Laudrup na wengine.

Usisahau makombe yake 11, yalimfanya ndiye kuwa kocha bora zaidi Barcelona. Alishika nafasi hiyo hadi alipopitwa na Guardiola ambaye ni mwanafunzi wake.

Nilipomuona kwa mara ya kwanza na kumueleza shida yangu, akaniambia angependa tuzungumze kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Wakongwe wa Barcelona wangecheza Aprili 11, nikamsikiliza.

Siku ilipofika nilikuwa pale, kuangalia mechi na kuzungumza naye. Niliona wengi wakiwa ‘busy’ na wachezaji wengine, bado nilitaka kuzungumza na Cruyff ambaye alionekana mtulivu na mwenye ushirikiano. Kabla ya mechi, alinifuata na kuniambia angefurahia kama tutazungumza tena baadaye.

Mwisho akasema, wakati mwingine anafurahia kutozungumza kwa kuwa anapenda zaidi kufurahia maisha kwa vile amekuwa ni mgonjwa, hivyo wakati wa furaha anapenda furaha.

Nilipomuuliza anaumwa nini, alisema: “Kansa, ni ugonjwa mbaya sana. Ukikukuta kusalimika ni nadra, nalijua hili.”

Nilishindwa kuendelea kumuuliza, lakini nikataka kujua kama tutazungumza tena. “Inawezekana, lakini kwa sasa hapana, maana naona vizuri niendelee kujumuika na wenzangu kidogo. Tuungane kufurahia.”

Nilikaa naye muda mrefu kidogo na wenzake pamoja na wachezaji wengine, lakini mmoja wa rafiki zangu aliyeongozana na Barcelona, Rayco Garcia aliniambia Cruyff amekuwa akipenda zaidi kufurahia maisha na huzungumza mara chache sana.

Mazungumzo yangu naye yalikuwa kwa njia ya ujumuisho. Yaani tulizungumza pamoja na akaweza kusema mambo kadhaa lakini nilishangazwa mara nyingi na tabia yake ya kuzungumza mara kwa mara neno la “bora kufurahia maisha tu.”

Sikuwa nimeelewa vizuri, lakini baada ya kusikia taarifa za kifo chake juzi. Nimeumia utafikiri mtu niliyeishi naye miaka mingi. Ningeweza kuacha, lakini nimeona “tushee” hilo pamoja kwa kuwa hofu yangu kuhusu ugonjwa hatari wa kansa inazidi kupanda kwa wanamichezo na jamii nzima, vizuri tupime na kujua hali zetu.

Namuona mtu kama Abel Dhaira, kipa wa zamani wa Simba ambaye pia ni mshikaji wangu akihangaika na jana hali yake ilikuwa mahututi kutokana na ugonjwa wa kansa unaomsumbua.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic