April 6, 2016


Pamoja na mshambuliaji hatari wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma kuwa msaada mkubwa kwa Yanga kutokana na uwezo wake lakini ameibua sekeseke jipya kwa mabeki wa Ligi Kuu Bara kutokana na kadi nyingi nyekundu anazowasababishia.

Ngoma ambaye ameifungia Yanga mabao 14, mpaka sasa kwenye ligi kuu ameweka rekodi mpya ya kuwasababishia mabeki wa kati watatu kadi nyekundu kila alipokutana nao kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Katika michezo mitatu ya Yanga iliyopigwa kwenye uwanja huo dhidi ya Mbeya City, Simba SC na Kagera Sugar yote haikumalizika salama kwa wapinzani ambao walimaliza mechi wakiwa pungufu uwanjani na hiyo ilisababishwa na Ngoma aliyetokea kuunda safu nzuri ya ushambuliaji na Mrundi, Amissi Tambwe.

Katika mechi yao na Mbeya City, Tumba Sued alipigwa kadi nyekundu baada ya kugongana na Ngoma katika dakika ya 56 na kusababisha pengo kwa timu hiyo ambapo mwisho wa matokeo Yanga ilishinda 3-0.

Mechi dhidi ya Simba pia iligeuka chungu kwa Wekundu hao baada ya beki wao, Abdi Banda kupigwa kadi mbili za njano alizozipata kwa kumchezea rafu Ngoma. Katika mechi hiyo pia baada ya Banda kutoka mpira ukageuka na mwisho wa matokeo Yanga ikashinda 2-0.

Jumapili iliyopita, Ngoma alikuwa tatizo jingine pia kwa Kagera Sugar ambapo beki wao, Shaban Ibrahim Sunza, alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuzawadiwa njano mbili zilizosababishwa kwa kumchezea kindava Ngoma. Mechi hiyo pia Yanga ilishinda 3-1.

Lakini kingine ni kwamba katika mechi ambazo wapinzani wanakuwa pungufu inakuwa faida kubwa kwa Ngoma kwani lazima atupie isipokuwa alishindwa kufanya hivyo katika mechi ya Mbeya City pekee. Katika mechi hiyo mabao mawili yalifungwa na Amissi Tambwe na moja Thabani Kamusoko.

Alipotafutwa Sunza kuzungumzia kinachowasibu hasa mpaka wanapewa adhabu hizo kupitia kwa mchezaji mmoja ambapo alikiri kuwa inatokea hivyo kwa kuwa ni ngumu kumkaba Ngoma aliyejaaliwa vitu vingi kama straika mwenye kuijua kazi yake.


“Yule mtu ni msumbufu na siku zote mabeki hawataki wala kuona mtu kama huyo anaisumbua ngome yake ki-rahisirahisi, kwa hiyo lazima ukitaka kumkaba kwa nguvu na kumpunguza makali ndiyo unajikuta anakusababishia kadi,” alisema Sunza.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV