Simba imepanga kumrudisha straika wake Emmanuel Okwi kutoka Sonderjyske ya Denmark lakini itabidi itoboe mfuko kwa kutoa dau la dola 100,000 iweze kumsajili tena.
Fedha hizo ni zaidi ya shilingi milioni 215.7, ambazo Simba itabidi iilipe Sonderjyske ambayo imekuwa ikimpa nafasi finyu Okwi ya kucheza kikosi cha kwanza.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, amenukuliwa akikiri Simba kuwa na mpango wa kumrejesha Okwi kikosini na mazungumzo yanaendelea kati ya timu hizo.
Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema klabu hiyo ipo ‘siriazi’ kukamilisha usajili huo ili kurejesha heshima yake lakini inachelewa kufikia muafaka na Sonderjyske kwani dola 100,000 ni kiasi kikubwa kwao.
“Hali hiyo ndiyo hasa inafanya Okwi achelewe kutua Simba kwani fedha wanazotaka ni nyingi sana, sisi tuliwaambia tuwarudishie nusu ya zile tulizowauzia ambazo dola 110,000 wao hawataki.
“Hata hivyo, mazungumzo bado yanaendelea na mambo yatakapokuwa sawa basi Okwi atarejea tena Simba na tuna uhakika wa kumpata halafu tukamuuza tena kwingine,” kilisema chanzo hicho.
Simba ilimuuza Okwi kwa dola 110,000 (Sh milioni 237.2) lakini sasa inataka imnunue kwa dola 55,000 sawa na Sh milioni 118.6 ambazo zimekataliwa na Sonderjyske, badala yake wanataka dola 100,000.
0 COMMENTS:
Post a Comment