April 22, 2016
Licha ya kutolewa kwa jumla ya mabao 3-2 katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly ya Misri, juzi, kikosi cha Yanga kimewasili leo jijini Dar es Salaam kikitokea Misri na kupata mapokezi mazuri.

Yanga iliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere mida ya mchana na kupokewa na mashabiki wao walioonekana kuwa na furaha na siri kubwa ya furaha yao hiyo ni kile walichodai kuwa timu hiyo ilionyesha uwezo mzuri katika mchezo wa pili ambao ulimazika kwa Al Ahly kupata ushindi wa mabao 2-1.

   
ULINZI ULIKUWA MKALI UWANJANI HAPO WAKATI YANGA IKITUA.
   Kikundi cha mashabiki wa Yanga waliokuwa  wamevaa jezi za timu hiyo baadhi zikiwa na majina ya wachezaji wao, walikuwa wakicheza muda mwingi hali ambayo ilisababisha wananchi wengi kuchukua muda wao na kuwatazama kile walichokuwa wakikifanya.

Mara baada ya msafara huo wa Yanga kutokeza kwenye lango la kutoka ndani ya uwanja huo, walipokea kwa shangwe na baadhi yao walikuwa wakilazimishwa kudansi akiwemo kipa wa Yanga, Deogratius Munish ‘Dida’.

Mashabiki hao walikuwa wakipiga picha na wachezaji wakati wakielekea kwenye basi la timu huku wakiwa na furaha, wachezaji wengine waliokuwa wakifurahiwa zaidi na mashabiki ni Thaban Kamusoko na Donald Ngoma.


Baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hiyo imeangukia katika Kombe la Shirikisho Afrika ambapo huko imepangwa kucheza na Sagrada Esperan├ža ya Angola.

Yanga imefikia hatua hiyo kwa kuwa kanuni za Ligi ya Mabingwa Afrika zinaeleza kuwa timu inayotolewa katika Raundi ya Pili itashushwa mpaka kwenye Kombe la Shirikisho kucheza mechi mbili za mtoano na itakayosonga mbele itaingia katika robo fainali Hatua ya Makundi.

Droo hiyo ilipangwa jana mchana ambapo pia kuna jumla ya timu nane kutoka Ligi ya Mabingwa na nane kutoka Kombe la Shirikisho.
 


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV