April 23, 2016NIKIWA NA NEYMAR
Na Saleh Ally, La Coruna
WAKATI mwingine, mchezo wa soka ni kama wendawazimu ambao dawa yake huenda ni kuona sura ya mtu fulani, halafu ukawa huna haja ya kwenda kutibiwa katika hospitali yoyote.
Nilianza safari yangu kwenda Hispania Jumapili iliyopita nikiongozana na washindi wa  promosheni ya ‘Kwea Pipa Kwenda Spain na Azam Sports HD’ iliyokuwa chini ya runinga ya Azam TV.


Pamoja na usimamizi wa Azam TV na mwaliko wa La Liga ambao wanasimamia Ligi Kuu ya Hispania, nilikuwa najiuliza maswali mengi kama nitafanikiwa angalau kufanya mahojiano mafupi na nyota wa Barcelona kwa kuwa tungeona mechi yao dhidi ya Deportivo La Coruna katika Mji wa La Coruna.


Hata mawasiliano ya awali na watu wa La Liga, walionyesha wazi kwamba kuna ugumu mkubwa kuwapata nyota hao.
Sikujali sana, nilisema nitapambana angalau kuwauliza hata swali moja tu. Baada ya kufika, wenyeji wetu La Liga walikuwa wakarimu sana, tulishirikiana vizuri sana na walikuwa wamejiandaa kitaalamu kabisa.


Kuhusiana na swali langu la kujua kama itawezekana, jibu likawa ni lilelile, kwamba ni vigumu sana. Bado sikujali, nikasema nitaangalia uwezekano.


Pamoja na yote, wendawazimu wangu ulianza kupoa kidogo baada ya kuelezwa tutapata nafasi ya kuwa VIP kwa maana ya kuwa karibu na wachezaji hao.


DANI ALVES AKISAINI JEZI YANGU

Ingawa tulitembezwa kwenye Uwanja wa Raizor unaomilikiwa na Deportivo La Coruna, hadi vyumbani ambako wangekaa Lionel Messi, Neymar, Luis Suarez na wenzao lakini bado niliwaza siku ya mechi.

Kweli siku ya mechi nilipata nafasi ya kuwa karibu kabisa wakati Barcelona wakiingia vyumbani, pia Deportivo. Ilikuwa ni kama umbali wa hatua tatu hivi, ilikuwa furaha kubwa lakini bado wendawazimu wangu haukuwa umeisha kwa kuwa ningependa kumsikia mmoja wao akijibu swali langu.


Bado nina ndoto nyingi, lakini Neymar, Messi au Suarez au wengine, nani atajibu swali langu? Ndoto itaendelea na sikutaka kuifunga au kuweka lebo ya ‘The End’. 


Baada ya mechi, Barcelona waliokuwa ugenini walishinda mabao 8-0, yote nikiyashuhudia kwa utulivu kabisa nikiwa jukwaani baada ya kuwa nimepewa nafasi ya kuuchambua mchezo kupitia luninga ya La Liga. Hii ni heshima nyingine.
Lakini nayo haikuwa imemaliza wendawazimu wangu. 


Wenyeji wetu wakatupa nafasi ya mwisho, walikuwepo pia waandishi wa Hong Kong na Sweden ambao waliongozana na washindi kutoka katika nchi zao.

Wenyeji walisema kila mmoja na ujanja wake ili mradi afuate sheria. Tulitakiwa kuchagua kati ya sehemu mbili na huu ndiyo mfumo wa michuano ya kimataifa au ligi kubwa duniani.


Kwenda kwenye ‘press conference’ ambako makocha wanazungumza au mix zone ambayo wachezaji hupita na kila mmoja kuuliza swali. Njia rahisi ya kuwatega ilikuwa ni kubeba angalau kitu kama unaomba wakusainie.

Hata hivyo, mwenyeji mmoja alitukatisha tamaa na kusema, mara nyingi wachezaji wa Barcelona huwa ni wagumu kusimama katika mix zone. Nikaendelea kusisitiza kimyakimya, “kitaeleweka tu”.


Wakati wanakaribia kuanza kutoka, niliona hata waandishi wa hapa Hispania wakiwa wamejiandaa kwelikweli. Nao walikuwa na hamu nao na ilionekana wazi hawana nafasi ya kuwakaribia hawa watu. Ilinishangaza kidogo lakini nikaendelea kujifunza.

Walipoanza kutoka, swali langu la kwanza likaenda kwa Kocha Luis Enrique ambaye alikuwa muungwana sana.

Saleh Ally: Enrique unafikiri ushindi wa nane, utafuta matumaini ya Atletico Madrid na Real Madrid kupambana kuwaondoa kileleni?
 

Enrinque hakujibu, alicheka na akasogea karibu yangu kabisa. Akasaini jezi ya Barcelona na kunirudishia kalamu yangu, akatokomea. Nikabaki naishangaa ile saini.

Sekunde chache alitoka Javier Mascherano, huyu jamaa utafikiri bwana jela. Hakutabasamu wala kutuangalia waandishi. Kila mtu alitupa swali lake na ikawa kama zogo.

Saleh Ally: Ushindi wa 8-0 leo, unafikiri Barcelona imerudi kwenye reli?


LUIS SUAREZ AKISAINI JEZI YANGU

Hakukuwa na jibu na Muargentina huyo akakatiza utafikiri ananijua au anaishi Dar, huku akiwa kanipiga jicho kali. Kidogo nikaanza kuhisi mambo hayatakuwa mazuri. Niache tu au niendelee? Haachwi mtu hapa.

Kidogo Sergio Busquets huyu yapa, haraka nilinyoosha mkono na kumuuliza.


Saleh Ally: Hongera kwa mchezo mzuri leo, unafikiri Barcelona bado ina nafasi kubwa kuwa bingwa au presha ya Atletico Madrid na Real Madrid ni tatizo?

 
Busquets: Soka kila kitu lazima upiganie, yote yanawezekana. (Alisema huku akisaini jezi yangu ya Barcelona iliyo mkononi, hakuendelea kujibu, akasaini kwa waandishi wengine na baadhi ya washindi wa Tanzania na Sweden, akaondoka, mwisho alinirejeshea kalamu kwa kunishika bega maana nilimuachia mkononi).

Nilipogeuka, Gerard Pique ambaye siku hiyo hakucheza, naye alikuwa karibu yangu. Lakini hakujibu lolote, baada ya kumuita jina, alisogea na kusaini kwenye flemu aliyokuwa nayo Mfanyakazi wa Azam TV, Irada Kitonga, halafu huyoo akaondoka kwa kasi ya kimondo.
 NIKIMKABIDHI NEYMAR JEZI YANGU ANISAINIE

Mara, Luis Suarez alikuwa amefika karibu yangu kabisa akiongozana na mabaunsa wawili. Sijui kilichotokea alikuja na kusimama hatua moja mbele yangu.

Saleh Ally: Hongera kwa mechi, unafikiri mna muda mrefu kwenye reli na nafasi ya ubingwa iko kwa asilimia kubwa?
 
Suarez alitabasamu, akachukua kalamu mkononi mwangu. Akasaini jezi yangu, halafu akasema: “Ligi ni ngumu, kila mmoja ana nafasi, wote tunapambana.”


Aliendelea kusaini kwa watu wengi kuliko tulivyotarajia, alionekana ni mkarimu na huenda aliongoza kusaini kwa watu wengi na wengine akipiga nao picha. Kilikuwa kivutio kwangu maana namjua kama mtu mtukutu sana. 

SERGIO BUSQUETS AKINIRUDISHIA PEN YANGU, MIMI BUSY NA SELFIE....


DANI ALVES


SERGIO BUSQUETS AKISAINI JEZI

Mara Messi huyu hapa, ilionekana wengi walimsubiri kwa hamu. Kwani washindi walikuwa wakimuita kwa nguvu, waandishi walitupa maswali yao, hata wafanyakazi wa La Liga nao walitaka wasainiwe jezi au vitu walivyoshika mkononi. 

Lakini alipita kama daladala la Mbagala lililojaza hadi mlangoni. Mbele alisimama na kupiga picha na mtoto, huyo akiwa na mabaunsa watatu akaingia kwenye basi, mwe!

Wakati yeye anatoka, wengine wanapita kimyakimya, Neymar naye akatoka akiwa na mabaunsa wawili. Bado nilipata hisia kwamba angepita kimya.


Haikuwa hivyo, baada ya kusaini kwa watu wawili, mwandishi na mshindi, akasogea kwangu. Alisaini jezi yangu, halafu nikatupa swali.


Saleh Ally: Barcelona inayumba, bado haiko katika kiwango chake, unafikiri sasa imerejea tena na ina uhakika wa ubingwa?

 
Alicheka, halafu akajibu: “No English”, kwamba hazungumzi Kingereza na alikuwa amefika kama hatua tatu akiondoka. Alikumbuka aliondoka na kalamu yangu na kuwasainia watu wengine. Akarudi na kunipa, akaondoka zake.


Wachezaji kadhaa waliendelea kupita, nao walikuwa na kasi kubwa na hakuna aliyejibu maswali.

Maswali yenyewe yalikuwa ya kurusha kama mvuvi na ndoano anayoitupia mtoni tena wenye maji yenye kasi. Lakini hiyo ndiyo Mix Zone.


Kwa aina fulani niliona huenda wazimu ulizidi kwa kuwa nilitamani wajibu au nizungumze angalau na mmoja wao kama dakika 15 hivi, lakini haiwezekani ingawa wapo waliojibu, wapo waliobeza na nikajifunza kwamba bado inawezekana. Bado sijasimama, shughuli inaendelea hadi wendawazimu utakapopata dawa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV