May 13, 2016

TAMBWE
Bao kali alilolifunga mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe, juzi dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, Tanga, limemkuna Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm ambaye ametamka kuwa hilo ni bao bora la msimu wa 2015/2016 katika Ligi Kuu Bara.

Tambwe alifunga bao hilo katika dakika ya 85 likiwa ni la pili na hivyo kuiwezesha Yanga kushinda mabao 2-0 baada ya lile la kwanza kufungwa na Mtogo, Vincent Bossou.

Tambwe, raia wa Burundi, ambaye anaongoza katika orodha ya wafungaji wa ligi hiyo, alifunga bao hilo kiufundi na kuwa bao lake la 21.

Ilikuwa hivi, wakati Mbeya City wakipambana kusawazisha bao moja, wakiungwa mkono na mashabiki wao uwanjani hapo, Yanga ilikuwa ikionyesha kupigana kama vile inacheza fainali wakati tayari ilikuwa imeshatwaa ubingwa wa ligi hiyo. 

Akiwa mbele ya mstari wa katikati upande wa kulia, Tambwe alipokea mpira ukiwa juu, akaukontroo ukiwa hukohuko juu, wakati Mbeya City wakiamini atatoa pasi au ataupiga kama krosi, Tambwe alichukua maamuzi ya haraka na ambayo hayakutegemewa na wengi.

Tambwe alipiga shuti kali lililoonekana kama linapaa juu ya lango kisha likashuka chini na kuelekea wavuni. Kipa wa Mbeya City, Juma Kaseja alikuwa amesogea kwa mbele kidogo, alipojaribu kurudi nyuma ili audake mpira huo tayari ulishajaa wavuni.

Kuingia kwa bao hilo kuliwanyamazisha mashabiki wenyeji ambao baadhi yao walianza kuondoka kabisa uwanjani hapo huku wale wa Yanga wakishangilia kwa nguvu.

Pluijm amesema mbali ya kuwa ni bao la msimu, pia ameliweka kwenye rekodi zake za mabao bora ambayo yamefungwa Yanga yeye akiwa kocha.

Aliongeza kuwa anahitaji washambuliaji wa aina hiyo ambao wanafanya maamuzi sahihi katika wakati sahihi.

“Kati ya mabao ambayo ameyafunga Tambwe tangu ametua kuichezea Yanga, basi lile dhidi ya Mbeya City, ni bora zaidi ya yote na hili ni bao la msimu huu wa ligi kuu.

“Mabao mengi yamefungwa mazuri, lakini hili la Tambwe sijaliona tangu msimu huu umeanza, kiukweli kabisa anastahili pongezi za hali juu na hiyo imetokana na kujituma kwake na kutimiza majukumu yake ninayompa.

“Washambuliaji wa aina hii mimi ndiyo nawataka kwenye timu yangu, wale wanaojitambua na kutimiza majukumu yao ya ndani ya uwanja ya kufunga mabao yao,” alisema Pluijm.


Bao hilo limemwezesha Tambwe kuvunja rekodi ya mabao katika ligi kuu, kujua zaidi soma ukurasa wa 12 na 13.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV