JUMA ABDUL (KULIA).. |
Beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul amemkaribisha Hassan Kessy kwenye timu hiyo kwa kumchimba mkwara kuwa, amekuja kwenye timu yenye ushindani wa kupata nafasi kikosi cha kwanza.
Kessy alisaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea Yanga hivi karibuni kwa dau la Sh milioni 40 huku akisubiria mkataba wake uishe Simba mwishoni mwa mwezi huu.
Ujio wa beki huyo, utaongeza ushindani mkubwa kwa Abdul ambaye hivi sasa anaonekana kuwa katika kiwango cha juu katika kuzuia na kushambulia.
Abdul alisema anamkaribisha Kessy kikosini na anaamini uwezo wake utaimarisha kikosi chao msimu ujao lakini anatakiwa kupambana kila anapopata nafasi ya kucheza.
“Kessy ni rafiki yangu wa muda mrefu na ujio wake nimeufurahia, ninaamini utazidi kukiimarisha kikosi chetu katika msimu ujao wa ligi kuu na michuano ya kimataifa.
“Kessy anachotakiwa kukitambua hivi sasa ni kwamba, amekuja kwenye timu yenye ushindani mkubwa wa nafasi, hivyo ili upate nafasi ya kucheza ni lazima upambane ndani ya uwanja kila unapopata nafasi.
“Kwa mfano mimi nilivumilia sana, kama unakumbuka wakati ninakuja nilikutana na ushindani kutoka kwa Twite (Mbuyu) na Nsajigwa (Shadrack), nilivumilia nikapambana na kupata nafasi ya kucheza,” alisema Abdul.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment