Na Saleh Ally
HIKI ndicho kipindi ambacho timu nyingi zinapambana kuwapata wachezaji ambao zinaamini watazisaidia kwa ajili ya kupambana kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Suala la kusaka wachezaji wapya limekuwa na mambo mengi sana yanayojumuisha mjadala na uamuzi wa moyo wa wachezaji husika kama wanataka kujiunga na timu fulani au la.
Wacheaji wapya mara nyingi wanakuwa ni kipande cha kuongeza au kurekebisha kile ambacho kimekosekana katika msimu uliopita.
Kama timu inataka kupiga hatua kutoka ilipo, au inataka kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita lazima iangalie ilipokosea na inataka kufanya nini kusonga mbele.
Mara nyingi wakati suala hili linashughulikiwa, wadau wengi wamekuwa wakisisitiza kwamba wachezaji wanapaswa kuwa makini sana katika suala la uigiaji mkataba ili kuwa na uhakika na wanachokifanya kwa wakati husika au mwafaka.
Mikataba ni jambo muhimu kwa kuwa muunganiko wa wachezaji ana klabu wakati mwingine unakuwa hauna tofauti na ile hadithi ya “wapendanao”. Kawaida huanza kwa ladha tamu lakini kama kutatokea msigano, mwisho wake unakuwa ni wenye uchachu na machungu.
Mara nyingi, mikataba inakuwa mtetezi wa kila upande. Hivyo wanaowasisitiza wachezaji kuwa makini na mikataba ili wasije kuchuuzwa ukifikia wakati wa machungu, naungana nao mkono.
Lakini pia nina ushauri tofauti, kwamba katika mikataba basi kuwe na utaalamu wa juu wa uandikaji na klabu ziachane na kuandika mikataba ileile ya aina ileile tokea enzi zile.
Mikataba inaweza kugeuka msaada wa kumfanya mchezaji kukua au kubadilika. Inavyoandikwa inaweza ikawa sehemu inayombana kuendelea kukua au kupambana na hasa kama kweli uongozi unalenga afanye vizuri.
Mfano, mchezaji kuwekewa kwenye mkataba wake vipengele ambavyo vinaeleza kama wakitwaa ubingwa atapata kitu fulani kama motisha. Mfano mgawo wa kiasi fulani kutoka katika fedha za ubingwa au vinginevyo.
,
Mchezaji kuelezwa akiwa mfungaji bora, pamoja na kubeba kiatu na fedha kutoka kwa wadhamini wa ligi, klabu nayo itamlipa kiasi fulani kama sehemu ya kuonyesha kuukubali mchango wake.
Kingine ni mchezaji kuahidiwa mfano safari na familia yake kama ataibuka mchezaji bora mara nyingi zaidi katika kila mwezi. Mfano mchezaji bora wa Aprili, Mei, Juni na kadhalika.
Mikataba ya namna hiyo ndiyo imekuwa ikitumiwa na klabu kubwa kwa lengo kuongeza hamasa ndani ya vikosi vyao kwa kuwa wanajua ushindani ni mkubwa.
Klabu hizo ingawa zinafanya mambo mengi ni siri lakini zinajua, bado suala la mshahara pekee haliwezi kutosha. Kumbuka soka si kazi ya kukaa ofisini, mchezaji kila siku anapambana upya kwa maana ya kupigana kweli.
Morali yake inapaswa kuwa juu kuanzia mazoezini na kwenye mechi. Kumbuka suala la kuwajenga watu kisaikolojia linaweza likasaidiwa kwa kiasi kikubwa na morali, hili ni jambo muhimu sana.
Kawaida, klabu zimekuwa na mikataba inayofanana na ile ambayo wachezaji waliingia na klabu hizo katika miaka ya 1990. Kuna kila sababu ya kubadilika na kufanya mambo ambayo yataendana na hali hali au wakati tuliopo.
Morali ya mchezaji ni rahisi sana kuporomoka, pia ni rahisi sana kupanda hasa kama kutakuwa na mbinu nzuri tena ndogondogo kama hizo za kuingia mkataba wenye mkataba unaonyesha motisha lukuki na inakuwa ni zamu ya mchezaji mwenye kuchagua azipate au la.
Kila kitu kinabadilika kwa kasi sana katika dunia ya michezo na hasa soka. Vizuri viongozi wa klabu wakawa wabunifu zaidi na kuangalia njia sahihi za kupita badala ya kusimamia katika mazoea na kuona kila kitu kinakwenda, hivyo ni poa tu.
0 COMMENTS:
Post a Comment