June 3, 2016


Straika wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe ameutaka uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha unasajili kiungo mkabaji (namba sita), wa nguvu katika kipindi hiki cha usajili ambaye atakuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo ambayo imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Tambwe ambaye ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa na mabao 21, amesema Yanga inakabiliwa na tatizo la kubwa la kiungo mkabaji mwenye uwezo kupambana muda wote wa mchezo.

Alisema hali hiyo ndiyo imekuwa ikiisumbua timu hiyo katika mechi zake za kimataifa jambo ambalo uongozi wa timu hiyo unapaswa kulifanyia kazi katika kipindi hiki cha usajili.

“Tuna viungo wengi wazuri lakini bado tunahitaji kiungo mkabaji wa nguvu ambaye atakuwa anashirikiana vilivyo na mabeki wetu katika safu ya ulinzi.

“Uongozi wetu unatakiwa kuliona hilo na kulifanyia kazi katika kipindi hiki cha usajili kabla ya kuanza kushiriki michuano ya kimataifa ambayo itakuwa na ushindani mkubwa kutokana na aina ya timu tutakazokutana nazo,” alisema Tambwe.

SOURCE: CHAMPIONI

  

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV