July 25, 2016Na Saleh Ally
KESHO ni siku nyingine ambayo inaweza kugeuka mateso au furaha kuu kwa mashabiki wa Yanga kulingana na kikosi chao kitakachofanya kazi nchini Ghana.

Yanga imeshatua nchini Ghana na imefanya maandalizi yote ya mwisho kabla ya kuivaa Medeama katika mechi yao ya nne ya Kombe la Shirikisho hatua ya makundi.

Yanga imecheza mechi tatu, maana yake imecheza na timu zote tatu za Kundi A na imeambulia pointi moja na kubaki mkiani, jambo ambalo linawaumiza Wanayanga wengi ambao wamezoea kuiona Yanga ikiwa kileleni au kinara sehemu fulani.

Mechi ya kesho dhidi ya Medeama inaweza kubaki ndani ya uamuzi wa kikosi cha Yanga ambacho hakika kimejaribu kuonyesha soka safi katika mechi zote tatu, lakini umakini au nidhamu ya utekelezaji wa mambo ndiyo iliwaangusha.

Medeama wakiwa jijini Dar es Salaam, walionyesha soka safi kabisa dhidi ya Yanga na mwishoni mwa mechi nusura wafunge bao la pili, jambo ambalo lingekuwa ni kufunga kabisa mjadala kuhusiana na Yanga.

Lakini Yanga ndiyo waliopata nafasi nyingi zaidi za kufunga ambazo kama wangeweza kuzitumia, basi wangepata matokeo ambayo yangesimama upande wao na kuwabeba.
Siku chache zilizopita niliandika kuhusiana na Yanga kuingia katika hatua ambayo ni ya juu kwao, kwamba timu za Tanzania zilisahau hatua ya makundi katika michuano yoyote ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa kipindi kirefu sasa.

Yanga imeingia hapo, unaona inakuwa ni kama inachechemea. Ukiangalia mchezo wao, unaona wanakosa vitu vichache sana ambavyo ndiyo nguzo ya timu nyingi zenye uzoefu katika hatua hiyo.

Yanga ilitengeneza nafasi za kufunga ikicheza mechi ya kwanza na MO Bejaia tena ikiwa ugenini Algeria, haikuzitumia. Ikafanya hivyo tena dhidi ya TP Mazembe ikiwa jijini Dar es Salaam, ikafungwa bao lililoanzishwa na adhabu.

Hali kadhalika, mechi dhidi ya Medeama, ikatengeneza zaidi ya nafasi safi nne za kufunga, ikatumia moja na kuruhusu bao lililoanzishwa na mpira wa kona. Jambo jingine ambalo ni somo kwao.

Hata kama nafasi ya Yanga sasa ni finyu sana, lakini wana uwezo wa kucheza vizuri na kushinda ugenini. Yanga lazima waamini, walifungwa ugenini wanaweza kushinda ugenini pia. Wapinzani wao wakapata sare ugenini, bado wanaweza kufanya hivyo.

Hisia za mashabiki wengi, wanaamini Yanga itaumizwa au kung’atwa na Medeama kwa kuwa walionyesha kiwango kizuri. Wachezaji wa Yanga wakiamini hivyo, waterejea nyumbani na aibu.

Wakiamini wanaweza kupambana na kushinda na kama itashindikana kabisa, basi angalau sare basi wanaweza kuepuka kung’atwa na wenyewe wakawa ndiyo wenye meno na kumng’ata mtu.

Soka si mchezo unaokwenda kwa hesabu, kuwa kama ulitoka sare na fulani ukiwa kwako, basi hauwezi kumfunga kwao. Au kwa kuwa MO Bejaia iliifunga Yanga bao moja tu, basi ikitua Dar es Salaam lazima ifungwe nyingi.

Kila dakika 90 za mchezo, inategemea unazipanga vipi wewe na kwa kipindi kipi. Mimi ninaamini Yanga wakitulia, wakacheza soka safi kwa kuwa hawatakuwa na presha kubwa sana, wanaweza kabisa kubadili mambo na kuwaangusha Medeama kwao.

Medeama ni timu nzuri na ngumu, lakini kesho itakuwa inacheza chini ya presha ya mashabiki wake ambao pia wangependa kuiona inapata ushindi wa kwanza maana imeshafungwa na kupata sare mbili.

Presha hiyo inaweza kuwa msaada kwa Yanga ambayo itakuwa iko ugenini na inaweza kufanya chini juu ikiwezekana kuanza kufunga ili kuwaangushia Waghana hao presha kubwa zaidi na kumaliza mchezo mapema kabisa. 

Katika soka, kisichowezekana huwa kinawezekana. Anayedharauliwa anaweza kuwa mfalme ingawa kila kinachotokea iwe kizuri au kibaya, huwa uamuzi wa mhusika.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV