July 25, 2016



KOCHA MKUU WA SIMBA, JOSEPH OMOG


Huku benchi la ufundi la timu ya Simba likiendelea kuwafanyia tathimini baadhi ya wachezaji wake wa kimataifa wanaofanya majaribio ya kutafuta nasafi ya kusajiliwa kwa ajili ya msimu ujao, uongozi wa klabu hiyo unatarajia kushusha straika mpya kutoka nchini Ghana.

Kwa jinsi mipango ilivyo, straika huyo anatarajiwa kutua nchi leo au kesho na kwenda moja kwa moja mkoani Morogoro kuungana na kikosi cha timu hiyo kilichojichimbia huko kwa ajili ya maandalizi yake ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20, mwaka huu.

Atakapofika huko, straika huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mpaka tunaenda mitamboni, atafanyiwa majaribio na Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog ambaye anaendelea na harakati zake za kukisuka upya kikosi hicho.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa ujio wa straika huyo klabuni hapo umetokana na uongozi wa klabu hiyo kufanyiwa mipango na baadhi ya maofisa wa timu ya soka ya Medeama ambao waliwaomba wawatafutie mshambuliaji wakati  walipokuwa hapa nchini na kikosi chao kwa ajili ya mechi ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Yanga.

“Ni kweli kabisa kesho au keshokutwa Jumanne tunaweza kumpokea straika mpya kutoka Ghana ambaye anakuja kufanya majaribio na endapo ataonyesha uwezo wa juu utakaomridhisha kocha basi tutamsajili.

“Straika huyo tumefanyiwa mipango na baadhi ya viongozi wa Medeama ya Ghana ambao tuliwaomba watutafutie wakati walipokuwa hapa nchini na kikosi chao kwa ajili ya kucheza na Yanga katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele ili azungumzie suala hilo hakupatikana, lakini alipotafutwa makamu wa rais wa  klabu hiyo, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alipatika na alipoulizwa alionyesha mshangao kisha akauliza: “Nani kakwambia jambo hilo, hakuna kitu kama hicho, siku ile ya mechi ya tulikwenda kuwapongeza tu Medeama na hakuna kitu kingine tulichozungumza nao lakini kama kuna lolote itajulikana.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic