July 4, 2016Uongozi wa Klabu ya Simba bado unaendelea na harakati zake za kukisuka upya kikosi cha timu hiyo ili kiweze kurejesha heshima yake iliyopotea kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Katika kufanikisha hilo, uongozi huo leo hii au kesho unatarajia kumpokea beki mpya kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo na kama mambo yatakaa sawa basi watasajiliwa.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zinasema beki huyo anatoka katika timu ya soka ya Dynamos inayoshiriki Ligi Kuu ya Zimbabwe.

“Bado tunaendelea na harakati zetu za kukiimarisha kikosi chetu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ili tuweze tunafanya vizuri na kurudisha heshima yetu iliyopotea kwa muda mrefu.

“Mungu akipenda kesho (leo) tunatarajia kumpokea mchezaji mwingine wa kimataifa kutoka Dynamos ya Zimbabwe ambaye anacheza nafasi ya  beki.

“Hata hivyo, baada ya kufika tutamwangalia kwanza na kama kiwango chake kitatuvutia basi tutamsajili ili aweze kushirikiana na mabeki wengine tulionao kwa ajili ya kuiongozea timu yetu kufanya vizuri msimu ujao,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele hakuweza kupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila ya kupokelewa. Juhudi za kumpata Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe pia hazikufanikiwa.

Mpaka sasa Dynamos inashika nafasi ya tano katika Ligi Kuu ya Zimbabwe ikiwa imecheza mechi 12, imeshinda sita, imefungwa nne na sare mbili.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV