July 16, 2016


Na Saleh Ally
AZAM FC imeonekana kuamua kubadili mfumo kabisa na kuajiri makocha wapya kutoka nchini Hispania ambao wanachukua mikoba ya Kocha Stewart John Hall raia wa Uingereza na timu yake.

Kocha Mkuu ni Zeben Hernandez ambaye atakuwa na kazi ya kuiongoza timu yake kuhakikisha inaleta mabadiliko na baadaye mafanikio. Kawaida Azam FC ni klabu inayotaka mafanikio na si utani.

Hernandez ambaye amewahi kuinoa timu ya daraja la kwanza nchini Hispania ya Tenerife, ataongoza timu ya makocha wengine kutoka Hispania, Yeray Romero ambaye ni msaidizi wake.

Wengine ni kocha wa makipa, Pablo Borges na kocha wa viungo, Jonas Garcia. Daktari pia atakuwa anatokea nchini Hispania ili kukamilisha jopo zima kutoka nchini humo ambako soka lake linasifika kuwa ni la kuvutia.

Tangu makocha hao watue nchini kumekuwa na gumzo kubwa kuhusiana na ujio wao Afrika, tena Tanzania. Kwamba watayaweza mazingira? Huku wako wenye hofu na makocha kutoka Hispania ambao ni aghalabu kusikika wanafundisha katika bara hili.

SALEHJEMBE ilifanya juhudi za kumsaka Hernandez na kufanya mahojiano naye na ilikuwa ni lazima kuzungumza naye kwa msaada wa mtu anayezungumza Kihispania na Kingereza kwa kuwa kocha huyo, Kingereza kwa kiasi kikubwa kinampiga chenga.

SALEHJEMBE: Kwa muda huu mfupi ambao umeanza kazi Azam FC, unaweza vipi kuwatofautisha wachezaji wa Tanzania na wale wa Hispania?
Hernandez: Tangu nilivyokuwa nikiona na sasa nimefanya kazi kidogo, wachezaji wa Tanzania kama wengine wa Afrika wana vipaji binafsi, Ulaya zaidi ni uchezaji wa kitimu.

SALEHJEMBE:Ukiwaunganisha wachezaji wa Tanzania au Afrika na kuwa kama timu unaona watakuwa hatari zaidi ya Hispania au Ulaya?
Hernandez: Hilo ni suala la muda mrefu, maana unabadilisha kitu ambacho hakina tofauti na utamaduni, lakini ninaamini hivyo.

SALEHJEMBE: Mazingira ya Tanzania, hasa viwanja vingi ni duni. Soka la Hispania ni kutambaza mpira, huoni litakukwamisha?
Hernandez: Kabla ya kuja Tanzania, nimesoma kila kitu. Ninajua hilo na nimelifanyia kazi.

SALEHJEMBE:Labda fafanua ulivyolifanyia kazi?
Hernandez: Mimi na timu yangu ya benchi la ufundi, tuko katika utengenezaji wa timu itakayocheza katika mazingira yote. Viwanja vibaya na viwanja vizuri.

SALEHJEMBE:Azam FC inakumbana na ushindani mkubwa hasa kutoka Yanga na Simba, hii inazaa presha kubwa. Je, mmejiandaa na hilo?
Hernandez: Presha ya mashabiki ni kila sehemu, tumejiandaa. Tunataka kuwashawishi mashabiki wengi zaidi kuiunga mkono zaidi Azam FC kwa kufanya kazi nzuri, iwavute huku.

SALEHJEMBE: Tokea umeanza mazoezi, unaonaje mwenendo wa wachezaji kama uelewa na utekelezaji?
 Hernandez: Kwa kweli wanajitahidi, wanafanya kwa kiwango bora kabisa.

SALEHJEMBE: Unazungumza Kingereza cha shida, haivurugi mawasiliano yenu?
Hernandez: Mwanzo kulikuwa na ugumu, lakini sasa tunaenda vizuri kabisa, ndiyo maana nimesema ninafurahishwa.

SALEHJEMBE: Soka ya Hispania ina utamaduni wake, sasa umekuta kuna utamaduni mwingine au wa Kingereza, unataka kubadili kila kitu?
Hernandez: Kweli nitafanya mabadiliko, lakini kuna mambo nitayaheshimu mfano utamaduni wa Kitanzania hasa kwa kitu kinachofaa ambacho tutabadili taratibu.


SALEHJEMBE: Kuna tatizo la ulaji sahihi kwa wachezaji wa Kitanzania au Kiafrika. Umelifanyia kazi hili?
Hernandez: Tuna mtaalamu wa masuala ya chakula, kitu kizuri kwa mchezaji ni kumshikilia ndani na nje ya uwanja. Vizuri kujua anafanya nini na inakuwaje ingawa yeye mwenyewe kujitambua inakuwa bora zaidi.

SALEHJEMBE: Uliomba siku 15 kuangalia wachezaji, kipi umekiona? 
Hernandez: Kama nilivyosema mwanzo, wanajitahidi sana na wamenivutia.

SALEHJEMBE: Je, unataka kuongeza wachezaji katika nafasi zipi?
Hernandez: Mshambuliaji, pia winga ila nitaendelea kuangalia lakini waliopo nao wanajitahidi sana ingawa ninasisitiza lazima wajitume zaidi.

SALEHJEMBE: Hii ya kukata dola 50 kwa atakayechelewa, huoni ni nyingi sana, maana kwa shilingi ya Tanzania ni zaidi ya Sh laki moja? 
Hernandez: Atakayeona ni nyingi, ajitahidi zaidi kuwahi. Nidhamu ni msingi wa mafanikio katika kila kitu, ni lazima kuidumisha.

SALEHJEMBE: Umri wako ni miaka 32 tu, kwa hapa Tanzania unaonekana ni mdogo na hauoni kama umri unaweza kikwazo kwako?
Hernandez: Kazi si umri, kocha wa Rwanda ana umri chini ya hapa. Nafikiri kazi yangu ndiyo majibu ya matokeo.

SALEHJEMBE: Mashabiki wanakuita Guardiola (Pep kocha wa Manchester City), unalipokeaje hili jina?
Hernandez: Mimi? (kicheko), siwezi kukasirika, mimi pia navutiwa na kazi zake (Guardiola). Mara kadhaa nimehudhuria katika makongamano aliyofundisha huko Hispania lakini ningefurahi zaidi kuitwa jina langu hasa Zeben.

SALEHJEMBE: Mategemeo ya mashabiki wengi ni kuona Azam inapiga pasi kama za Barcelona. Hili litawezekana ukiwa na wachezaji ulionao?
Hernandez: Hapo kuna tatizo kidogo, Azam FC haiwezi kuwa Barcelona wakati haina Messi, Iniesta, Javier Mascherano na wengine. Hii ni Azam FC, ila watarajie mpira wa aina yake. Itacheza katika mfumo ambao utaitambulisha lakini si kuwa timu nyingine.

SALEHJEMBE:Umeanza mabadiliko, unafikiri utaweza kukamilisha mabadiliko hayo na kubeba makombe au msimu ujao upite ukiwa unafanya mabadiliko tu?
Hernandez: Hili litategemea zaidi wachezaji wameelewa haraka kiasi gani. Kama watafanya kila kinachotakiwa, kuchukua makombe inawezekana kabisa.


SALEHJEMBE: Azam FC ina sifa ya kulinda sana lango. Kwenye kushambulia haikuwa kali sana. Vipi umelifanyia kazi hilo?
Hernandez: Kama ni sinema, basi sterlingi ni mpira. Kuumiliki vema, kuutumia sahihi maana yake ni kupata mafanikio. Mimi na wenzangu tutabadili kila tunachoona tunataka kufanya hivyo ili tufanikiwe. Kufunga ni lazima pia kulinda ni lazima. Napenda kulinda kwa kumiliki mpira badala ya kukaa langoni. Ukilinda huku unamiliki, nani atakufunga wakati mpira unao wewe!

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV