July 30, 2016


Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, ameogopa na kusema msimu ujao wa Ligi Kuu Bara unaweza kuwa mgumu kwao hata kutetea ubingwa kwani wana uchovu wa kucheza mechi nyingi mfululizo.

Cannavaro amesema hayo wakati Yanga ikiwa bado kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.
Tofauti na timu nyingine za ligi kuu ambazo zilipumzika baada ya ligi hiyo kumalizika Mei, mwaka huu, Yanga yenyewe iliendelea na mechi za Kombe la Shirikisho na itacheza hadi Agosti 24, mwaka huu.

Yanga inatarajiwa kumaliza mechi zake za Kundi A za Kombe la Shirikisho kati ya Agosti 23 na 24, mwaka huu wakati msimu ujao wa ligi kuu ukianza Agosti 20, yaani siku tatu au nne nyuma yake.

Cannavaro alisema msimu uliopita walipata muda wa kupumzika na wakatetea vizuri ubingwa wa ligi kuu, lakini safari hii hawajapumzika na mambo yanaweza kuwa magumu.

“Tangu ligi imalizike hatujapumzika, halafu ukiangalia msimu mpya unatarajia kuanza, hii itatufanya tuwe na wakati mgumu wa kutetea ubingwa wetu kwani tutakuwa tumechoka,” alisema Cannavaro.

Kuhusu Yanga kutofanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho, Cannavaro alisema: “Kinachotuangusha ni kushindwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani, wenzetu wakicheza kwao wanapata matokeo mazuri lakini kwetu inakuwa tofauti.

“Hili ni somo kwetu na kwa kuwa msimu ujao tutashiriki tena, basi tutafuta makosa yetu, benchi la ufundi nadhani limeona linatakiwa kusajili wachezaji wa aina gani hasa katika michuano hii ya kimataifa.”


Yanga inashika mkia katika kundi lake ikiwa na pointi moja tu huku TP Mazembe ikiwa kinara na pointi 10 ikifuatiwa na Medeama na MO Bejaia ambazo kila moja ina pointi tano.

1 COMMENTS:

  1. Yanga wanaweza kuwa kwenye advantange kuliko timu nyingine kwa sababu licha ya mechi mfululizo kukupa mazoezi ambayo yanakufanya uwe fiti kuliko timu nyingine bado Yanga wamefanya mabadiliko kidogo sana kwenye kikosi ukilinganisha na timu nyingine na hivyo kufanya timu kufahamiana zaidi......zaidi ya yote huwezi kufananisha mechi walizocheza Yanga na zile a Simba dhidi ya Moro Kids kwani zimewapa uzoefu mkubwa sana...........ikumbukwe hii ndiyo ajira na hata kama wasingeshiriki kimataifa bado haimaanishi wangelala hadi ligi ianze

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV