Na Saleh Ally
WAKATI wa tuzo za Mwanasoka Bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2015-16 zilizofanyika jijini Dar es Salaam, Mgeni Rasmi alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba.
Mwigulu alizungumza mambo mengi lakini moja lilikuwa ni kuhusiana na uzalendo kwa Watanzania kushindwa kutambua hata umuhimu wa bendera ya taifa lao.
Alieleza kitu kilichotokea wakati wa mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya Yanga dhidi ya TP Mazembe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Mashabiki waliokuwa kwenye jukwaa la Simba walizomea wakati bendera ya taifa ikipandishwa, halafu wakashangilia kwa nguvu wakati bendera ya DR Congo ikipandishwa.
Mwigulu alionyesha kushangazwa sana na hilo na mwisho akasema hivi: “Inapandishwa, bendera ya Tanzania, si ya Yanga, inapandishwa mlingotini. Wanasimama mashabiki wa Yanga wanashangilia.
“Wengine kule wanazomea, bendera ya Tanzania si ya Yanga! Halafu inapandishwa DRC, wanasimama Watanzania walioizomea bendera ya Tanzania wanaishangilia bendera ya DRC! Hili kwa wazazi wetu waliopigania uhuru, wakikuona unafanya hivyo watatokwa na machozi.”
Mwigulu alizungumza maneno haya akionyesha kuumizwa kwa kuwa Watanzania walishindwa hata kutambua bendera ya nchi yao, wakaizomea kwa kuwa tu hawafurahishwi huenda na mafanikio ya Yanga au Yanga kuwa wawakilishi wa taifa.
Mwanamapinduzi maarufu wa Kirusi, Vladmir Lenin amewahi kusema: “You can not make a revolution in a white gloves.” Kwamba hauwezi kufanya mapinduzi ukabaki na mikono misafi, au ukabaki msafi.”
Neno “White” hapa linatumika kwa maana nyingi sana. Unajua, unapotaka kusaidia kupatikana kwa mabadiliko, kamwe usitegemee utafanikiwa ukiendelea kuonekana ni mtu mwema au mtenda haki kwa kuwa lazima ukinzane na misimamo ya wengi ambao watakuwa na sababu nyingi sana kutokana na mazoea.
Hakika lazima watakulaumu na kupinga kwa kuwa wako ambao ni wazabizabina walio tayari kuona wanaisaliti nchini yao kwa lengo la kumuudhi mtu au kundi la watu fulani. Utaifa unakuja baadaye.
Watanzania wengi ni watu wasiojua thamani ya bendera ya nchi yao. Ndiyo maana ni aghalabu kuona hata wanajipaka rangi za bendera hiyo au kuvaa jezi za Taifa Stars kwa wingi na kuishangilia.
Kuna baadhi ya athari zilijengwa kipindi cha utawala wa awamu ya kwanza, pale ilipoonekana mwananchi hatakiwi kuonekana akiwa amebeba bendera kwa kuwa ni kwa watu maalum.
Wakati Mwigulu anashangazwa na tukio hilo moja lililotokea akiwa uwanjani. Mimi, kwa kipindi kirefu sasa nimekemea rundo la matukio ya kijinga kama hayo na kuwaeleza ukweli ambao wamekuwa wakiwazomea wachezaji wa timu ya taifa kwa kuwa ni Yanga naye ni Simba au anawazomea wa Simba kwa kuwa yeye ni Yanga.
Vita hii na wadau wachache tumepigana hadi kwa kiasi kikubwa inaanza kuyeyuka na angalau watu kuanza kuona si sahihi au anayethubutu kufanya hivyo, kuonekana hayuko sahihi.
Mwigulu kushangaa kama mwanadamu halikuwa jambo baya, lakini ninaona hakupaswa kuishia kushangazwa na kuliacha likapita tu, badala yake alitakiwa kukemea na kuagiza kuzikwa kwa upuuzi huo ambao unaweza kumshangaza hata mdudu mdogo anayetambaa kama angeweza kutambua kinachofanyika.
Hakuna haja ya kumlea Mtanzania mjinga ambaye anashindwa kutambua Utanzania wake. Baadaye anakwenda mbali zaidi na kuudhihaki utambulisho wa nchi yake ambao ni utambulisho wa jina na ufahari wake kuwa ni mtu anayetokea wapi.
Kama Mtanzania anashangilia bendera ya DR Congo na kuizomea ya Tanzania, huyo ni juha. Kama Mtanzania anaweza kuidhihaki bendera ya nchi yake akiamini ya DR Congo ndiyo sahihi ni mwendawazimu ambaye anapaswa kukemewa na si kuelezwa kwa kubembelezwa.
Ushabiki wa mpira ni furaha na una mipaka yake. Utaifa ni namba moja, utaifa ndiyo uhai wa nafsi wa kila mmoja wetu kwa kuwa ndiyo utambulisho wako.
Katika michezo, kuna watu wengi sana ambao kamwe hawathamini kuhusiana na utaifa, wako wanahabari wamelipigania sana hili na “gloves zao haziwezi kuwa white” hata kidogo. Kwa kuwa unaowakosoa, kula kila njia ya kutaka kuonyesha ni wakosaji.
Katika hafla hiyo, Mwigulu alimzungumzia Mbwana Samatta kwamba ni mfano wa uzalendo maana alifunga bao katika mechi akiwa TP Mazembe, akakimbilia bendera ya Tanzania. Hii ni kwa kuwa Samatta alijifunza kwa wengine anaocheza nao, wanajua maana ya uzalendo.
Hapa nyumbani kuna shida kuu ya somo la uzalendo. Wengi hawajui, lakini hawajui kama hawajui. Wengi hawaitendei nchi haki lakini wanataka iwatendee na wakipungukiwa kidogo, lawama ni kubwa kuliko kivuli cha mwili wa tembo.
Angalia kwenye Kamati ya Olimpiki (TOC), kila siku ni lawama na majungu na utaona suala la kufaidika kwa wahusika fulani kuliko utaifa inapofikia michezo hasa ya Olimpiki. Unakumbuka mara ngapi Tanzania hupeleka viongozi wengi kuliko washiriki wa michezo?
Kwenye riadha, migogoro ni ya kimaslahi, mchezo unaporomoka na wale wakongwe wenye sifa kuu katika mchezo huo kama Juma Ikangaa na Filbert Bayi hawaelewani. Kwenye netiboli, mwisho Mama Anna Kibira amekata tamaa.
Katika soka, Mungu atusaidie! Chuki, majungu, husda ndiyo msingi. Kila mmoja anataka achukue chake mapema huku akitangaza maendeleo yanakuja.
Uzalendo haupo tena na takwimu zinaonyesha kwenye uzalendo kidogo, maendeleo ya kitaifa kwa maana ya maendeleo ya umoja huwa chini.
Viongozi wa soka, zaidi wanaangalia maslahi yao. Hakuna anayejali kuhusiana na mafanikio ya taifa ndiyo maana kuna hadithi nyingi za kusikitisha kama ile ya mkufunzi wa Chama cha Soka Oman (OFA) aliyemba kuja kufundisha makipa, ikiwa pia anatoa mipira na mavazi. Mmoja wa mabosi wa shirikisho hilo wakati huo, akataka kujua naye atafaidika vipi!
Leo viongozi wa shirikisho hilo, hawataki kukosolewa. Wanachofanya hadi sasa wanaamini hakijawahi kutokea kwa maana ya ubora. Kwa kuwa mioyo yao haina uzalendo inakuwa ni vigumu kung’amua kuwa wanaharibu.
Mapenzi kwa nchi yetu hakuna kwa wanamichezo wengi. Mapenzi yamejaa kwenye fedha na kila mmoja anayepata nafasi ya kuongoza, anatamani kutajirika au kupunguza ukali wa maisha, si kuendeleza michezo.
Mwigulu ni mwanamichezo, najua anaelewa mengi haya. Suala la kushangazwa na kusikitishwa wala asingepaswa kulipa nafasi, badala yake angepaswa kulitolea maelezo na amri kwamba kuzomea bendera ya nchi yetu si sahihi hata kidogo.
Ninaamini, neno “iwe mwanzo na mwisho” lingefaa. Neno “atakayebainika, atachukuliwa hatua kali iwe mfano” lingekuwa bora zaidi na ikiwezekana hatua zichuliwe. Sitaki kumfundisha kazi Mwigulu lakini nasisitiza kumkumbusha, Watanzania wengi hasa huku kwenye michezo, wanapenda kuamrishwa ili watekeleze.
Kuzomea bendera ya nchi ni usaliti, kushangilia wachezaji wa timu ya taifa kwa kubagua timu ni ujinga. Viongozi kuendelea kulitafuna taifa kupitia michezo ni uhujumu uchumi na kuukanyaga uzalendo. Viongozi wa nchi, Mwigulu na wengine, pambaneni kulimaliza hili, hakuwezi kuwa na maendeleo bila ya uzalendo na kwa kuwa mmeliona, siasa ipungue katika hili na hao wanaojifanya hawajui, waanze kuona shida yake kwa kuwa hakuna demokrasia ya kuzomea taifa lako kwa kisingizio cha michezo.
SOURCE: CHAMPIONI
This comment has been removed by the author.
ReplyDeleteunajua 'ujuha' ni ujuha pale mtu anapokurupuka kukemea jambo bila kujua chanzo cha jambo hilo.
ReplyDelete