July 22, 2016



Na Saleh Ally
MKUU wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Simba, Haji Sunday Manara, sasa yuko New Delhi nchini India ambako anapata matibabu ya macho.

Jicho la kushoto la Manara halioni hadi anaondoka nchini wakati lile la kulia, limepunguza uwezo wake wa kuona kwa zaidi ya asilimia 50, hii si hali nzuri kwake ambapo mbali na matibabu, tumekuwa tukimuombea kwa Mwenyezi Mungu amsaidie apone na kurejea katika hali yake ya kawaida.

Wakati Manara akiwa hospitali, kuna tukio lilitokea la wanachama na mashabiki wa Yanga kuchangishana kupitia mitandao mbalimbali ili wawe sehemu ya waliochangia Manara afanikiwe katika matibabu hayo.

Fedha zilizokuwa zinatakiwa kufanikisha matibabu ya Manara, zilikuwa ni zaidi ya Sh milioni 22 kwa kuwa imeelezwa anaweza kubaki India angalau kwa wiki mbili hadi tatu ili mambo yaende safi.

Viongozi wa Simba hasa wale wa Kundi la Friends of Simba, wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kuhakikisha hilo la matibabu linafanikiwa, lakini wapo mashabiki na wanachama wa Simba, baadhi walichanga pia kuhakikisha mambo yanafanikiwa na Manara anatibiwa.

Wakati michango inakwenda, wanachama wa Yanga kupitia mitandao ya kijamii walichangishana Sh 1,055,000 na kumkabidhi Manara. Hawa waliochanga ni Wanayanga na wengi ni wenye maisha ya kawaida ambao walijitolea kwa maana ya mioyo yao ya upendo na si uwezo mzuri kifedha au utajiri.

Wanayanga hao, walimchangia Manara ambaye amekuwa akiwananga redioni na kwingineko, lakini walifanya hivyo wakiangalia zaidi ubinadamu na si ushabiki ambao zaidi ni utani badala ya chuki.

Baada ya kuchangishana, baadhi ya Wanayanga hao walifunga safari hadi nyumbani kwa Manara na kwenda kumkabidhi fedha hizo. Manara alishindwa kujizuia na kutoa chozi wakati wawakilishi wao daktari, Nassor Matuzya na Jerry Muro ambaye huonekana ni mpinzani wake walipokuwa wakimkabidhi.

Pamoja na kutoa shukurani nyingi, Manara aliweka mbwembwe zake za utani na kusema atakaporejea India akiwa amepona vizuri, basi Yanga watamkoma. Hali iliyosababisha wote wacheke wakiashiria furaha ya kukutana na mazungumzo yao.

Wanayanga hao ambao ni wachache, wamekuwa wawakilishi wa wengine wengi na unaweza kuwaita ni Wanamapinduzi wanaotaka kurejesha maana ya utani wa Yanga na Simba ambazo zilikuwa timu moja kabla ya kugawanyika mwaka 1936.

Yanga na Simba ni ‘tumbo moja’, lakini mwendo wa maisha yao katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ni tatizo kubwa. Yanga hawafiki kwenye misiba ya watu wa Simba na Wanasimba hawataki kwenda kusaidia matatizo ya Wanayanga!

 Maana ya utani ambao hutafsiriwa kwa upendo, haipo tena! Kila upande unauona mwingine ni kama adui, jambo ambalo si sahihi hata kidogo.

Wengi wanaopotosha na kutaka kuuvunja ule utamaduni wa ushabiki wa klabu hizo, ni wale waliochipukia mwanzoni mwa miaka ya 1980 na wamekuwa wajuaji na wasiotaka kujua kilichopita au kilichozifikisha klabu hizo hapo zilipo.

 Hauwezi kukana mchango wa wazee wa Yanga na Simba, waliopo na waliotangulia mbele ya haki. Walikuwa watu imara na waliosaidia kukua na kupatikana kwa mashabiki wengi zaidi ya waliopo sasa.

Suala la ushirikiano, kuzikana, kushiriki pamoja matatizo au furaha kama harusi na mambo mengine, yalikuwa ni mambo muhimu.

 Waliokwenda nyumbani kwa Manara kumpelekea mchango wao, wamezaliwa upya na kurejea kwenye usahihi wa maana ya utani wa jadi wa Yanga na Simba. Wanaondoka kwenye huu utani wa sasa unaoweza kuuita “utani wa jadi” kwa kuwa watu wamewekeana uzio badala ya kukaribiana na kuwa pamoja.

Hongera kwao kwani vijana wengi wa kipindi uelewa wao ni mdogo kuhusu utani wa jadi, lakini hawa wameonyesha utani bora unaweza kurejea tena na kuachana na “utani wa jadi” uliotawala kipindi hiki.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic