August 17, 2016

Bonge la mechi ya kisasi leo linatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa kuwakutanisha mabingwa watetezi Yanga watakaovaana na wapinzani wao, Azam FC kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.

Mechi hiyo hatachomoka mtu kwa kuwa ni lazima timu moja ipate ushindi aidha kwa dakika tisini au kwenye mikwaju ya penalti.


Katika mechi hiyo Azam wataingia uwanjani kwa kazi moja pekee ya kulipa kisasi baada ya mara mbili zote walizokutana katika Ngao ya Jamii kufungwa.

Wataingia uwanjani wakiwa na benchi jipya la ufundi linaloongozwa na Mhispania, Zeben Hernandez aliyetua nchini hivi karibuni akirithi mikoba ya Muingereza, Stewart Hall aliyesitishiwa mkataba wa kuendelea kukinoa kikosi hicho.

Akizungumza na Championi Jumatano kocha wa Yanga, Hans van Pluijm alisema kikubwa yeye anataka kuendeleza rekodi yake ya kuchukua mataji kwa kuanza hili la Ngao ya Jamii.

Pluijm alisema, taji hilo la Ngao la Jamii anataka kulichukua ili atengeneze mwanzo mzuri katika kulitetea taji lao la ubingwa wa ligi kuu na Kombe la FA, hiyo ni kutokana na mabadiliko makubwa ya wachezaji waliyoyaonyesha hivi karibuni baada ya kupata uzoefu mkubwa.

"Ninataka kuanza na mwanzo mzuri kwa kuchukua Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, licha ya kukabiliwa na changamoto moja ya wachezaji wangu kutumika kwa kipindi kirefu bila ya kupumzika tofauti na timu nyingine ambazo zimepata muda wa kupumzika.



 
"Kama unavyojua tupo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo tulikosa muda kabisa wa kupumzika, lakini hiyo hainipi hofu kutokana na maandalizi niliyoyafanya ya kikosi changu, tutatumia uzoefu tulioupata kwenye michuano hiyo kuwafunga Azam.

"Ninafurahi mabadiliko makubwa ya kikosi changu kwa kuanzia safu ya ulinzi iliyokuwa ikikosa umakini katika kuokoa mipira ya krosi na kona na kusababisha kuruhusu mabao, lakini nafurahia mabadiliko makubwa hivi sasa," alisema Pluijm.

Hata hivyo, Yanga watakuwa na pigo kubwa leo kwa kuwa itawakosa mastaa wake watano ambao wanasumbuliwa na majeraha ambao ni Kelvin Yondan (jicho), Obrey Chirwa (goti), Juma Abdul (misuli), Ally Mustapha (kidole) na Vincent Andrew (nyonga).

  



  Kwa upande wa kocha wa Azam, Hernandez yeye ameweka wazi kuwa ana uhakika mkubwa wa kuifunga Yanga kwenye mchezo huo kutokana na maandalizi mazuri aliyoyafanya.

"Nisingependa kuzungumzia sana mechi ya Yanga kwani ninaamini kuwa, jitihada zangu na mafunzo yangu ninayowapa wachezaji wangu itazaa matunda, lakini natambua ya kuwa Yanga ni timu kongwe na inacheza vizuri.

"Kikubwa ninaamini nitashinda kwenye mchezo huu kutokana na kile ninachowapa wachezaji wangu na kikubwa, nimeweka mkazo kwenye baadhi ya sehemu kwa kuwapa mbinu mbadala zitakazotupa ushindi," alisema Hernandez.

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic