August 27, 2016


Kiwango kinachoonyeshwa na mshambuliaji wa Genk ya Ubelgiji, Mtanzania, Mbwana Samatta, kimemkuna Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm na mwisho akafafanua kuhusiana na uwezekano wa siku moja staa huyo kucheza katika timu za Ligi Kuu England.

Nahodha huyo wa Taifa Stars, amekuwa msaada mkubwa kwa sasa katika timu hiyo ya Genk na kufanikiwa kufunga mabao manne katika mechi nne alizoichezea timu hiyo kwenye msimu mpya wa 2016/17 na kuwa kileleni mwa msimamo wa wafungaji bora wa ligi hiyo mpaka sasa.

Pia juzi Alhamisi Samatta aliiongoza Genk kutinga kwenye michuano ya Europa League.

Pluijm, raia wa Uholanzi, ameeleza kwamba Samatta ni mchezaji wa kuigwa kwa wachezaji wengi wa Tanzania, si kwa uchezaji tu bali hata nidhamu na tabia yake uwanjani na vingine vingi ambavyo vimempa mafanikio na kufikia hapo alipo.

“Samatta ana spidi, ubora, akili, tabia njema na ni mfano mzuri kabisa wa kuigwa na wachezaji wengi wa Tanzania kama wanahitaji kufika alipofika Samatta, bado nayaona mengi mazuri yapo mbele yake kutokana na heshima ya mpira aliyonayo.

“Nimesikia pia akihusishwa kuweza kuishawishi Manchester United siku ikitokea amekutana nayo kwenye Europa League. Soka la England siyo kitu chepesi, lakini niseme kwamba kijana (Samatta) anapambana sana na mpira una njia zake.

“Kiuhalisia mpira hauna mipaka, kama unajitahidi na kuweka nia, utafika popote unapotaka, cha msingi Samatta aongeze bidii zaidi kwa hapo alipofika na atacheza ligi nyingi kubwa,” alisema Pluijm, kipa wa zamani wa timu ya taifa ya Uholanzi.

SOURCE: CHAMPIONI 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic