August 6, 2016

HIMID
Kiungo mkabaji wa Azam FC, Himid Mao, ameingia matatani baada ya kutuhumiwa kumtwanga ngumi askari wa usalama barabarani.

Taarifa zinasema, Mao ambaye ni mtoto wa mwanasoka wa zamani, Mao Mkami 'Ball Dancer' aliyechezea Pamba ya Mwanza, anatuhumiwa kumtwanga ngumi askari huyo wa usalama barabarani katika eneo la Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

SALEHJEMBE ilifanya mawasiliano na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga ambaye alisema amepata taarifa hizo pia.

“Kweli imetokea, nimeelezwa mchezaji huyo anashikiliwa kwenye kituo cha Stakishari, lakini kwa kuwa sasa ni suala la jinai, vizuri ukiwasiliana na RPC,” alifafanua Kamanda Mpinga.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni zilizaa matunda na awali akasema ana taarifa lakini apewe muda kidogo.

Alipopigiwa baadaye alisema kweli kumetokea tukio hilo na kufafanua chanzo ni mwendo kasi wa gari ambayo alikuwa akiendesha Himid.

“Ni tukio la asubuhi, inadaiwa huyo mchezaji wa Azam alikuwa katika mwendo wa kasi, askari alipomsimamisha wakati akihoji ilitokea kupishana kauli, ndipo mchezaji huyo alipomkwida shati lake na kumtwanga ngumi ya usoni.

“Nimeambiwa amemjeruhi vibaya usoni na hivi sasa mchezaji huyo anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Sitakishari kwa ajili ya mahojiano zaidi ila taarifa za kina juu ya suala hilo bado hazijanifikia.

"Nasubiri ripoti ya maandishi ili niweze kujua eneo sahihi lilipotokea tukio hilo, jina la mtuhumiwa ambaye ni mchezaji wa Azam pamoja na askari aliyepigwa,” alisema Hamduni.

Kwa upande wa Azam FC, Msemaji wao Jaffar Idd Maganga maarufu kama Mbunifu, alikiri kutokea kwa suala hilo. Lakini akataka apewe muda.

"Nimeelezwa kuna kitu kimetokea kuhusiana na Himid, lakini bado si taarifa rasmi na maofisa wetu linashughulikiwa. Hivyo siwezi kuzungumza lolote," alisema.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV