August 27, 2016

MIGI

Kiungo wa Azam FC, Mnyarwanda, Jean Mugiraneza ‘Migi’, amefunguka kuwa licha ya kuanza kwa sare katika mchezo wa kwanza dhidi ya African Lyon, anaamini wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwani hakuna timu itakayoweza kuwazuia, zikiwemo Simba na Yanga.

Azam ambayo ililazimishwa sare ya 1-1 na African Lyon, leo Jumamosi inatarajiwa kucheza na Majimaji kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar.

Migi ambaye ni kiungo wa timu ya taifa ya Rwanda 'Amavubi', alisema kuwa wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa msimu huu kutokana na ubora wa kikosi walichonacho msimu huu tofauti na msimu uliopita.

“Kiukweli matokeo mabaya ya mechi iliyopita siyo kigezo ambacho kinaweza kutufanya tushindwe kufanya vizuri katika ligi ya msimu huu kwa sababu kila kitu kipo sawa kwa upande wetu, zaidi ya wachezaji wenye kujituma kwa nguvu zote ili kuweza kufikia lengo.

“Angalia mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, tulikuwa nyuma kwa mabao mawili lakini mwalimu akafanya mabadiliko tukafanikiwa kusawazisha na kuwafunga, sasa sioni kitu ambacho kinaweza kutufanya tukashindwa kuwa mabingwa wa msimu huu wa  ligi kwani hata hao Simba pia wanafungika licha ya kwamba wapo vizuri,” alisema Migi.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV