August 27, 2016


Huku Yanga kesho Jumapili ikitarajiwa kushuka uwanjani kupambana na African Lyon katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu, jana mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji alifanya kikao kizito cha dakika 270 na wachezaji wa kikosi hicho.

Kikao hicho maalum kilifanyika kwenye ofisi za bilionea huyo zilizopo jengo Quality Plaza jijini Dar. Kikao hicho kilianza saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:30 Mchana.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zimedai kuwa, kikao hicho kilikuwa maalumu  kwa wachezaji pamoja na viongozi wa benchi lao la ufundi ambapo walipata kujadili mambo mbalimbali yanayowahusu, likiwemo suala la ushiriki wao kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ambao wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutetea ubingwa wao.

“Ni kweli kabisa wachezaji wetu walikuwa na kikao na mwenyekiti kwa ajili ya kuzungumza mambo mbalimbali yanayowahusu lakini pia ushiriki wao katika michuano ya ligi kuu.

“Kama unavyojua siku chache zilizopita walipatwa na hofu kubwa baada ya taarifa kuwa mwenyekiti anataka kuachana na timu kutokana na kuchoshwa na matusi ambayo amekuwa akikumbana nayo tangu siku aliyotangaza kutaka kuikodi timu yetu.

“Kutokana na hali hiyo, pia ametumia mkutano huo kuwaondoa hofu hiyo waliyokuwa nayo wachezaji wetu na amewataka wapige kazi kwani ushindani msimu huu ni mkubwa na yeye yupo nao bega kwa bega kuhakikisha wanawatimizia mahitaji yao yote, ikiwa ni pamoja na stahiki zao wanazostahili kupewa kulingana na makubaliano yao,” kilisema chanzo hicho cha habari na kuongeza:

“Mambo sasa yamekaa sawa, hivyo ile hofu ya kufanya vibaya msimu huu ikiwa ni pamoja na mchezo wetu wa kwanza dhidi ya African Lyon imeondoka, hivyo Wanayanga tushikamane pamoja ili kuhakikisha hatuvurugani tena.”

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit ili aweze kuzungumzia suala hilo, hakuweza kupatikana kufuatia simu yake ya mkononi kuita tu bila ya kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi hakuweza kujibu.


Hata hivyo, walipoulizwa kuhusiana na suala hilo, baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ambao waliomba kutotajwa majina yao gazetini walisema: “Taarifa hizo ni za kweli kabisa kwani ilikuwa tukutana naye jana (juzi) lakini baadaye tulipewa taarifa kuwa amechoka na leo (jana) ndiyo tumekutana naye."

SOURCE: CHAMPIONI 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV