August 26, 2016


HAPA NDIYO VALDEBEBAS...

Na Saleh Ally aliyekuwa Madrid
REAL Madrid ya Hispania ndiyo klabu tajiri kuliko zote duniani. Niliamua kujifunza mambo ikiwa ni pamoja na kutafuta mengi yanayoihusu.

Moja ya kitu kikubwa ambacho Real Madrid inamiliki ni Sports Center au sehemu maalum ya mazoezi ambayo ni kubwa kuliko zote duniani.

Sehemu huyo inajulikana kwa jina la The Ciudad Real Madrid yaani Mji wa Real Madrid. Iko katika eneo la Valdebebas, kama kilomita 15 hivi kutoka katika ya Jiji la Madrid.

Miaka 13 iliyopita, eneo hili la Valdebebas lilikuwa kama kijiji, lakini sasa ni maarufu sana kutokana na Madrid kujenga eneo kubwa kwa ajili ya mazoezi, kambi na kadhalika.

RAMANI YA VADEBEBAS BAADA YA KUINGIA KWENYE ENEO HILO...

Eneo la Valdebebas si mbali sana na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Barajas na aliyechukua uamuzi wa kununua eneo hilo alikuwa ni Rais wa Real Madrid, Florentino Perez ambaye alionekana kama hakuwa na maana wakati huo.
Ukubwa wa eneo hilo ni mita za mraba milioni 1.2 na hadi sasa Madrid wametumia takribani mita za mraba 100,000 tu kutokana na maendeleo kadhaa ambayo yamekuwa yakiendelea.

Nilipofika hapo, nilikuta ukiongezwa uwanja mmoja wa mazoezi lakini jengo kubwa ambalo ofisi za wafanyakazi wa Real Madrid zilizopo kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu katikati ya mji zitahamishiwa hapo. 


Kama haitoshi hata ofisini ya Rais Perez, nayo itahamishiwa hapo na kufanya Ciudad Real Madrid kuwa na shughuli zote za kisoka kuanzia uwanjani hadi ofisini ambazo zitakuwa zikifanyika hapo.

Ndani ya eneo hilo ambalo si rahisi kuingia kutokana na ulinzi mkali, lina sehemu tatu kubwa za kuegesha magari, ikianza ile ya timu kubwa ambayo ni magari ya akina Cristiano Ronaldo, Gareth Bale na wenzake huegeshwa wakati wao wakiwa kazini au katika eneo hilo.


Upande mwingine wa maegesho ni kwa ajili ya wafanyakazi wote wa eneo hilo ambao wanakadiriwa kufikia 300. Maegesho ya tatu ni sehemu ambayo wanayatumia zaidi wageni wakiwemo wazazi wa vijana walio katika eneo hilo wakiendelea na mafunzo. Kwani kwa wiki mara mbili hufika kuwajulia hali na kupewa maendeleo yao.

Rasmi mwaka 2005, ndiyo eneo hilo lilianza kutumika. Ndani yake kuna viwanja vya nyasi bandia na vile vya majani ya kawaida na vimetenganishwa.

HUU NI MMOJA WA UWANJA AMBAO HUTUMIWA NA TIMU YA WAKUBWA YA REAL MADRID.

Mfano upande wa timu ya wakubwa chini ya Zinedine Zidane, kuna viwanja viwili, nyasi bandia na majani ya kawaida. Hii ni kutokana na mahitaji ya kocha. Kuna sehemu wametengewa uwanja mkubwa ambao unaweza kugawanywa na kuwa mdogo mara nne au mara mbili.

Ndani ya majengo ya eneo hilo kuna ofisi kubwa kwa ajili ya akademi, vyumba kwa ajili ya vifaa, vyumba zaidi ya viwili kwa ajili ya mafunzo kutumia mitambo ya video ambayo huweza kuichambua mechi kwa kuikatakata au kuonyesha makosa, kama ambavyo huona kwenye runinga wakati wachambuzi wakifanya kazi zao.

MOJA YA VIWANJA NDAI YA ENEO LA VALDEBEBAS

Kuna hospitali ndogo ambayo hutumika kwa wachezaji wapya kufanyiwa vipimo, waliopo kutibiwa na kuna mgawanyo. Hospitali imegawanywa upande wa timu ya wakubwa na timu za vijana ambao wako wengi zaidi.

Ndani ya eneo hilo, kuna jumla ya viwanja 13 vikiwemo vya nyasi bandia na vile vya majani ya kawaida. Mmoja ni uwanja wa mechi tu ambao umepewa jina la mmoja wa mashujaa wa Madrid, Alfredo di Stefano.
Uwanja huo hutumiwa kwa ajili ya kuchezea mechi tu kwa timu ya wachezaji wa akiba wa Real Madrid maarufu kama Castilla.

CHUMBA HIKI HUTUMIWA KWA AJILI YA KUWAPA VIJANA MAFUNZO YA SOKA KUPITIA DARASA

Madrid wamewahi kutamba kwamba kikosi cha Castilla kinaweza kuchukua ubingwa katika ligi ya nchi yoyote duniani hata England. Wachezaji wa kikosi hicho ni kati ya wanaolipwa fedha nyingi sana za mishahara.

Uwanja huo wa Alfred di Stefano una majukwaa na ndiyo mkubwa zaidi na inawezekana ingekuwa hapa nyumbani ungeweza kutumika hata kwenye ligi, kwani kwa ubora unaonekana ni bora hata kuliko wa Azam Complex ambao kwa hapa nyumbani, ni uwanja bora zaidi kati ya ile inayomilikiwa na timu binafsi.

SEHEMU YA VYUMBA VYA KUBADILISHIA NGUO VYA VIJANA WA REAL MADRID NDANI YA VADEBEBAS

Hoteli:
Kuna hoteli kubwa ambayo pia imegawanywa katika sehemu mbili. Upande wa timu kubwa ambayo sifa yake ni ya nyota tano. Halafu upande wa timu za vijana ambayo ni nyota tatu. 

Wachezaji kuanzia chini ya miaka saba, yaani U7, U8, U10 na kuendelea hadi U20, wako kambini wakiishi hapo na wazazi hufika kuwatembelea. Ndani ya kambi hiyo kuna vijana wapatao 285 na ukifika tu, unapewa nafasi ya kupiga picha mbele ya sura zao.

HIKI NI KIWANJA CHA NDANI, KAMA KUNAKUWA NA MVUA KUBWA AU KIPINDI CHA BARIDI KALI.

Maisha yao ni hapo, wanakula hapo na wanaendelea na maisha yao. Huku wazazi wakiwa wanapewa nafasi ya kufika kuwatembelea mara mbili kwa wiki, au zaidi kama itahitajika.

Niliomba kufikishwa upande wa kambi ya wakubwa hasa vyumbani, jambo ambalo lilishindikana kwa kuwa timu hiyo ilikuwa safarini katika mechi ya ufunguzi wa La Liga dhidi ya Real Sociedad, hivyo nikapata nafasi ya kutembezwa upande wa timu za vijana. Ingawa walinikubalia kutembea kwenye viwanja vya mazoezi vya timu kubwa.

MMOJA WA WALIMU WA TIMU ZA VIJANA.

Siku hiyo, Ronaldo hakuwa mazoezini kwa kuwa ni majeruhi, lakini upande wa uongozi ukasisitiza, haukumpa taarifa kuhusiana na ujio wangu, hivyo si jambo la kistaarabu kwa utamaduni wao. Pia anahitaji utulivu ‘ku-fucus’ namna ya kurejea. Wakati naingia alikuwa amelala kwa muda wa saa moja, ili akiamka aendelee na mazoezi mepesi chini ya daktari akiwa pamoja na beki wa timu hiyo, Contreao.

Upande wa vijana, niliingia kwenye mgahawa wa wageni, baada ya hapo, kocha wa vijana chini ya miaka 11, ndiye aliyefanya kazi hiyo ya kunizungusha katika maeneo mbalimbali tukianza na hospitali maalum kwa ajili ya timu za vijana, mabafu yapatayo nane, kila moja lina uwezo wa kuchukua watu 14 wakioga pamoja, pia kuna kuna vyumba maalum kwa ajili ya mechi, viko viwili.

RAMANI YA CIUDAD REAL MADRID, YAANI MJI WA MICHEZO WA REAL MADRID
Ubora wa vyumba hivyo ni maradufu hata vya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambao ni bora kuliko viwanja vingine vyote nchini na ukanda wote wa Afrika Mashariki.


Pia, nikapelekwa hadi kwenye uwanja wa ndani. Huu hutumiwa na vijana wakati baridi kali na pia timu kubwa nao wana uwanja wao.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic