Na Saleh Ally
MOJA ya gumzo kubwa lililowahi kutawala England katika masuala ya usajili ni mshambuliaji Fernando Torres kuhama Liverpool na kwenda kujiunga na Chelsea.
Torres alijiunga na Chelsea kwa kitita cha pauni milioni 50 na kuweka rekodi ya juu ya usajili. Mioyo ya watu wa Liverpool ikawa chini, yenye huzuni kwa kuwa kipenzi na mwokozi wao alikuwa amekimbia.
Mafanikio yanaendana na juhudi ambayo ndiyo inayotangulia. Na kila anayefanikiwa kwenye juhudi yake, hutaka kupiga hatua. Torres alitaka hayo, ndiyo maana ilikuwa ni lazima aende Chelsea hata kama alikuwa akiipenda zaidi Liverpool.
Kawaida, akiondoka aliyekuwa staa lazima huzaliwa staa mwingine. Unaona Laudit Mavugo alikuwa staa wa Vital’O ya Burundi, alikoondoka lazima atapatikana mwingine.
Lakini ana kazi ngumu na kubwa ya kutengeneza jina upya akiwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, akiwa na timu yake mpya ya Simba ambayo imemsaka kwa siku nyingi huku zikitengenezwa filamu za kila aina kuhusiana na ujio wake.
Torres alikuwa maarufu Liverpool na England, lakini akashindwa kuuendeleza umaarufu huo akiwa na Chelsea, hadi akajikuta akikubali kupelekwa kwa mkopo AC Milan, angalau kujaribu mazingira tofauti.
Mavugo amekuwa gumzo sana, lakini bado Wanasimba na wapenda soka wengine wangehitaji kuona sababu ya msingi ya uongozi wa Simba kupambana kumpata angalau kwa misimu miwili mfululizo bila ya mafanikio, lakini wakaendelea kumsaka.
Mavugo anaonyesha alijiamini zaidi, akaamini Simba si saizi yake, akaamua kwenda kufanya majaribio Ulaya lakini amerejea tena Simba, baada ya kuona mambo yamefeli huko ughaibuni.
Ubora wake ni upi? Hakuna takwimu zinazombeba kuonyesha ni mchezaji hatari sana kuliko wengine ambao Simba ingeweza kuwapata.
Mfano, amekuwa akikaa benchi timu ya taifa ya Burundi na wakati mwingine akiwekwa benchi na Amissi Tambwe ambaye wakati anatua Simba alikuwa mfungaji bora wa Kombe la Kagame.
Mavugo amekuwa akikaa benchi katika kikosi cha timu ya taifa ya Burundi, maana yake amekuwa si chaguo la makocha wengi wa timu hiyo.
Kwangu ninaona Mavugo atakuwa ni mshambuliaji wa kawaida ambaye ili afanikiwe Simba, ni lazima ajitume kwa kiwango cha juu zaidi na kwa weledi wa juu pia.
Hakuna takwimu zinazomlinda Mavugo na kuonyesha ni mtu hatari sana au ni mshambuliaji atakayekuwa tishio kama Yanga ilivyomsajili Donald Ngoma ikiwa imeona kazi yake ilivyo kwa kuwa walikutana uwanjani.
Kwa kifupi, Mavugo ana deni kubwa kwa Wanasimba ambao pia wana hamu kuu ya mafanikio na watakuwa wamechoshwa na maumivu ya “nafuu” au “ilibaki kidogo”.
Maana yake, Mavugo na hata wenzake waliojiunga na Simba, watakuwa na kazi ya kuonyesha kuwa Simba hawajakosea kuhusiana na wao.
Hakutakuwa na chaguo la lugha au maneno mengi kwa Mavugo dhidi ya Wanasimba zaidi ya kuonyesha mchango mkubwa katika kikosi cha Simba. Na hasa iwe kwa ufungaji wa mabao.
Inawezekana asifunge akawa ni mtu aliyesababisha mabao mengi zaidi. Pia huo utakuwa ni mchango mkubwa wa kuonyesha mhusika amelenga kuona kikosi kinafanya vema.
Lakini nitoe angalizo kwa Wanasimba, lazima wakubali kuwa mchezaji ni kama binadamu, anapaswa kuingia katika mambo kadhaa. Mfano kuzoea mazingira au kuzoeana ana wenzake.
Mavugo hawezi kuanza leo na kuweza kila kitu, vingine vitahitaji kuzoea taratibu kabla ya kuanza kuonyesha kitu sahihi alichonacho.
Wanachama na mashabiki wa Simba, walikuwa sehemu ya kuusaidia uongozi kuamini kiungo Pierre Kwizera hana kitu. Msimu uliopita ndiye Mwanasoka Bora wa Rwanda akiwa na Rayon Sports.
Hivyo, hata kama Mavugo atakuwa na kazi ya kuonyesha kweli anastahili kuwa gumzo katika usajili wake, basi mashabiki wa Simba, benchi la ufundi na uongozi wampe nafasi kama aliyopewa Torres na Chelsea, hadi ikafikia kila mmoja akakubali, kweli anastahili kuondoka.
Si lazima ifikie hadi kama hiyo ya Torres, huenda Simba wasiwe na uvumilivu huo lakini bado wanaweza kukumbuka, hata wachezaji wao nyota wa zamani kama Emmanuel Okwi hawakutamba ndani ya nusu msimu au msimu mzima.
Kwa mazoezi ya jana tu, inaonekana Simba wana mchezaji ambaye akituliza akili yake basi ana uhakika wa kuwa msaada mkubwa katika kikosi hicho.
Awali, nimezungumzia kutofanya vema au kutokuwa chaguo namba moja katika kikosi cha Burundi. Lakini Mavugo anaweza kuitumia Simba kufanya vema zaidi na baadaye kuwa tegemeo hata timu hiyo ya taifa lake.
Lazima kuwe na hali ya kuaminiana kutoka kila upande. Rekodi na historia inaonyesha wachezaji wengi waliokuwa gumzo, wengi hushindwa kufanya vema.
Wanaoshindwa kufanya vema hutokana na presha ya gumzo lao na mategemeo kutoka kwa wanaomsubiri.
Kama kila upande utashindwa kutulia, basi mara moja husababisha mchanganyiko na mgawanyiko na mwisho ni kutokuwa na kuelewana kunakozaa kutengana.
0 COMMENTS:
Post a Comment