August 6, 2016

MANJI
Unaweza kusema leo ni siku ya neema Yanga, kinachotakiwa ni wanachama kupitisha mabadiliko, klabu iwe kampuni kwa mfumo wa hisa na bilionea yuko tayari kumwaga Sh bilioni 65 kununua hisa 55%.

 Tajiri huyo yuko jijini Dar es Salaam, shabiki wa Yanga na Mkurugenzi Mkuu wa Kundi la Wanachama wa Yanga la G20, Abbas Shentemba, amesema kama mwenyekiti wao Yusuf Manji yuko tayari, watamuachia kama la, basi bilionea huyo, atachukua timu.

Manji ameitisha mkutano wa dharura leo kuzungumza na wanachama wa Yanga na moja ya ajenda ni kufanya uboreshaji wa katiba ambayo itawapa nafasi wanachama kuamua ni namna gani wanataka klabu yao iendeshwe.
“Kwanza niseme nampongeza sana Manji, amejitolea sana na wanachama na mashabiki tunapaswa kuheshimu hili. 

Anatoa fedha zake nyingi, wanaohoji vitu vidogo lakini hawahoji timu inaishi vipi na wachezaji wanapataje mishahara yao nawashangaa.

“Kikubwa watu wajitokeze kwenye mkutano na kusikiliza. Kwangu ningewasihi kesho wakubali mabadiliko, Yanga ijiendeshe kikampuni na kuuza hisa. Mimi nina mfanyabiashara anayetaka kununua hisa kwa dola milioni 30 (takriban Sh bilioni 65).

“Yeye anataka hisa za Yanga asilimia 55 tu. Zilizobaki zitakuwa za wanachama wengine. Yuko tayari kujenga uwanja na yuko tayari kuwaachia Yanga majengo yao.

“Ndiyo maana nimesema hivi, kama Manji atataka kutoa fedha, basi tutamwachia kwa kuwa ni mtu aliyejitolea sana, lakini kama hawezi, basi huyu tajiri yupo na yuko tayari kabisa,” alisema Shentemba na kuongeza:

“Hata suala la kujenga uwanja, mimi naweza kusaidia kuwalipa fidia watu wa eneo la Jangwani, pia eneo la Kigogo Sambusa.”

Salehjenbe: Huyo bilionea yuko wapi, ni nani hasa?
Shentemba: Wanachama wa Yanga wakikubali mabadiliko, nitamtangaza.

Salehjenbe: Vipi hautaki kumtangaza wamjue mapema, asije akawa mamluki?
Shentemba: Mimi ni Yanga, namjua ni Yanga, siwezi kukubali kuiuza Yanga kwa mamluki.

Salehjenbe: Labda ni raia wa Tanzania, asili yake?
Shentemba: Ni Mtanzania, asili yake Tanzania. 

Kama kweli hili litapita, yatakuwa ni mapinduzi makubwa kwenye soka nchini kwa kuwa wiki iliyopita wanachama wa Simba walikubali kupitishwa kwa mabadiliko na mfanyabiashara Mohammed Dewji maarufu kama Mo akasema wakikubali anataka kununua hisa asilimia 51 kwa kitita cha Sh bilioni 20.

Kama kweli alichokisema Shentemba, maana yake mnunuzi wa Yanga atakuwa ametoa mara tatu na ushee kununua hisa zinazokaribiana na zile ambazo ametangaza kutaka kununua Mohammed Dewji ‘Mo’ ndani ya Simba.
Suala la mfumo huu ni moja ya ajenda zitakazojadiliwa kwenye mkutano wa leo utakaofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar lakini pia kuna hofu kwa baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji kwamba wanaweza kutupiwa virago hali ambayo imefanya waanze kuushambulia uongozi wa Yanga wakitaka kujua mambo kadhaa ambayo hawayaelewi.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga naye alizungumza na kuonyesha kushangazwa na wajumbe wa kamati ya utendaji kuhoji kwenye vyombo vya habari.


“Ninazungumza na kila mjumbe, wangeweza kuniambia. Tulifanya kikao mimi nilimwakilisha mwenyekiti, lakini vipi leo tulumbane kwenye vyombo vya habari? Sehemu sahihi ya kusemea kwa wajumbe wa kamati ya utendaji ambao ni viongozi, wanajua ni wapi,” alisema Sanga.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic