August 29, 2016



Na Saleh Ally
KAWAIDA ninapenda sana kuweka kumbukumbu ya mambo mengi kwa ajili ya matumizi ya baadaye au sehemu ya elimu tu.

Hivi karibuni, nilimfanyia mahojiano mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali ambaye alizungumza mambo mengi sana, ninaamini ilikuwa makala nzuri iliyowanufaisha wasomaji wa gazeti hili.

Kwa kuwa ilikuwa ni siku chache baada ya Simba Day, mzee Dalali pia alizungumzia mambo kadhaa kuhusiana na kikosi cha Simba ambacho siku ya tamasha hilo kiliitandika AFC Leopards ya Kenya kwa mabao 4-0.

Ushindi wa Simba uliamsha mwamko wa matumaini mapya miongoni mwa mashabiki wake ambao walichoshwa na timu yao kutofanya vizuri kwa miaka minne mfululizo, inamaliza ligi bila ya kombe hata moja au kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa katika miwili ya mwisho chini ya uongozi wa Ismail Aden Rage na miwili ya mwanzo ya Evans Aveva. 

Sasa wanachotaka ni mafanikio na kweli wana hamu ya mafanikio, lakini mzee Dalali aliwaeleza kwamba katika soka, siku zinatofautiana.

Kwanza aliwakumbusha kutokuwa na matumaini kupita kiasi, kuachana na kuamini kwamba kwa ushindi wa siku ile au katika mechi za kirafiki, basi Simba haifungiki tena.

Baada ya sare ya Simba dhidi ya JKT Ruvu juzi Jumamosi, maana yake sasa kikosi hicho kina pointi nne baada ya mechi mbili. Jambo ambalo Wanasimba wengi wanaonekana kutofurahishwa nalo na wengine walianza kulaumu mitandaoni, baadhi wakimtupia lawama kocha au benchi la ufundi, mara hivi mara vile, ilimradi kila mmoja anajua sana.


Hii ikanifanya nikumbuke kauli ya mzee Dalali, kwamba Simba ni timu na kila siku haiwezi kushinda. Laudit Mavugo ni binadamu, hawezi kucheza kwa kiwango cha juu kila siku. Itafikia siku atakosea au kucheza katika kiwango cha chini, hali kadhalika kikosi kizima cha Simba.

Sasa tayari imetokea, alichokieleza mzee Dalali wiki chache zilizopita kimeanza kutokea. Tayari baadhi ya mashabiki wa Simba, wameanza kusukuma lawama ambazo ninaamini kabisa hazina msingi na wasipoangalia watajichanganya.

Kwani Simba, wanaamini wana ubora upi hadi kupata pointi moja waone si saizi yao au wamepunjwa sana? Wana kipi hasa cha kuona hakuna kama wao au wao kupata sare na JKT ni kama dhambi!

Simba ndiyo kwanza imeanza ligi, haijapoteza hata mechi moja katika mbili na ina pointi nne. Ina kocha mpya na wachezaji wapya rundo. Unapozungumzia kocha mpya maana yake ni mabadiliko ya mfumo na kuunganisha kikosi.

Lazima kila mmoja ajue, mechi za kirafiki ni tofauti na ligi. Hata uchezaji wake au maandalizi na mipango kwa makocha inakuwa tofauti. Kwa Wanasimba waliokwenda uwanjani au kushuhudia kwenye runinga, waliona kikosi chao kilicheza vizuri na walikuwa na matatizo mawili, matatu.

Kung’ang’ania mpira bila sababu kwa wachezaji, umaliziaji na pia wachezaji kuonekana kama wana presha kubwa hali inayopoteza utulivu wao.

Nimeliona hili tatizo kwa Yanga kwa kipindi kirefu. Huenda baada ya kuwatokea, walishindwa kulirekebisha kutokana na presha kuendelea kuwa kubwa kutoka kwa mashabiki au kwingineko.

Simba wanalazimika kujipanga na kuwa makini sana na hilo, la sivyo litawaangusha na watacheza mechi nyingi wakishambulia sana lakini mwisho wataishia kwenye sare au kufungwa wao na sifa yao itakuwa ni soka safi la kushambulia sana bila matunda baada ya dakika 90.

Ushauri wangu ni kwa mashabiki kuachana na kubeba presha za kishabiki na kuziingiza kwenye kikosi chao, hali inayoweza kusababisha timu hiyo kujawa na hofu na baada ya hapo kuzidisha kukosea au kuteremsha utendaji wa wachezaji.

Kwa wachezaji wa Simba nao wanapaswa kutoingia sana mitandaoni na kuonekana wanajali au kufuatilia kila kinachosemwa, mwisho watajiangusha na kujijaza presha zaidi.


Mzee Dalali aliliona hilo mapema kwa kuwa anajua soka, leo na jana ni tofauti. Vema wengine wakajifunza kupitia jicho hilo la mzee Dalali.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic