September 10, 2016



Leo Jumamosi Azam FC inacheza ugenini na Mbeya City katika Ligi Kuu Bara, kocha wa timu hiyo Zeben Hernandez amesema ni lazima washinde leo halafu wajiandae kupata pointi tatu kwa Simba.


Baada ya mchezo wa leo na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Azam itarejea jijini Dar es Salaam kujiandaa na mechi yake dhidi ya Simba itakayochezwa Septemba 17, mwaka huu.

Azam ina pointi saba sawa na Mbeya City na timu hizo zimelingana mabao ya kufunga na kufungwa, hivyo kuleta ushindani wa aina yake katika mchezo wa leo.

Zeben, raia wa Hispania, aliliambia Championi Jumamosi kuwa, anajua mechi ya leo ina presha kubwa kwa timu zote lakini atahakikisha wanashinda ili kujiimarisha kileleni.

“Tunajua wapinzani wetu wana kikosi kizuri ambacho kitacheza nyumbani kwa lengo la kushinda, ili kushusha presha ni lazima tupate matokeo bora tukiwa huku Mbeya.

“Nitahakikisha tunashinda mechi yetu hii halafu tushinde mechi inayofuata (na Simba) ili tuwe katika nafasi nzuri zaidi kwenye ligi,” alisema Zeben.

Kwa upande wa Kocha wa Mbeya City, Kinnah Phiri, raia wa Malawi, akizungumzia mchezo huo alisema: “Tumejiandaa vizuri kwa mechi yetu na Azam na tumejipanga vilivyo kuhakikisha tunaibuka na ushindi kwani tuna faida ya kucheza nyumbani.

“Nimewaona Azam katika mechi dhidi ya Prisons, ni timu nzuri lakini nimeshajua jinsi gani ya kukabiliana nao na kuwafunga ili tuweze kukaa vizuri kileleni.”

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic