Yanga, jana ilitarajiwa kuzungumza na kiungo mshambuliaji wake wa zamani Andrey Coutinho mambo ambayo hakuna upande uliokubali kuweka wazi, lakini mchezaji huyo amesema mambo yakienda tofauti atawashawishi Haruna Niyonzima na Thabani Kamusoko wa timu hiyo aondoke nao.
Coutinho raia wa Brazil alitua nchini Jumatano wiki hii na Championi linajua kuna harakati za chinichini za Yanga kutaka kumrudisha kikosini japokuwa wote hawakuwa wazi kuthibitisha hilo.
Lakini Coutinho aliliambia Championi Jumamosi: “Nazungumza na Yanga leo (jana) kama mambo yakiwa tofauti, nitawashawishi Niyonzima na Kamusoko tukachezea soka Asia, naamini tutafanikiwa.”
Coutinho amemaliza mkataba na Rakhine United inayoshiriki Ligi Kuu ya Myanmar ya barani Asia licha ya awali kusema hafikirii kuongeza mkataba wa kuichezea timu hiyo, kama Niyonzima na Kamusoko wakimkubalia ataongeza mkataba.
“Sitaki kuongeza mkataba sababu timu haichezi kwa ushindani na hakuna malengo ya ubingwa lakini kama Niyonzima na Kamusoko wakikubali kujiunga na klabu ile nami nitasaini mkataba.
“Nitazungumza nao (Niyonzima na Kamusoko) ili twende wote Myanmar endapo maongezi yangu na Yanga hayatakaa vizuri,” alisema Coutinho ambaye msimu uliopita ameifungia Rakhine mabao 10.
Coutinho, leo Jumamosi anatarajiwa kuwepo Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuitazama Yanga ikicheza na Majimaji mechi ya Ligi Kuu Bara.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment