September 13, 2016

Baada ya kuambulia kipigo cha aibu cha mabao 2-1 kutoka kwa Alves, timu ambayo imepanda daraja msimu huu, wababe wa Hispania, Barcelona, leo watakuwa kwenye uwanja wao wa Camp Nou kukipiga na Celtic lakini hasira zao zipo, juu.

Kocha wa Barcelona, Luis Enrique hana mpango wa kupumzisha wachezaji au kufanya mzunguko ili wengine wapate nafasi badala yake amepanga kuanzisha kikosi kamili.

 Tangu kuanza kwa msimu huu washambuliaji watatu wa Barcelona, Lionel Messsi, Luis Suarez na Neymar hawajaanza pamoja katika mechi moja.

Taarifa kutoka ndani ya Barcelona zinaeleza kuwa wanachowaza kwa sasa ni fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo itafanyika Juni 3, 2017 kwenye Uwanja wa Millennium.

Katika mchezo uliopita wa La Liga, Barcelona iliwapumzisha mastaa wake kadhaa na kujikuta ikipata kipigo hicho ambacho hakikutegemewa na wengi.

Akizungumza kuhusu mchezo huo wa leo, Enrique alisema: “Celtic ina wachezaji wenye vipaji, ni klabu yenye historia kubwa, napenda ufundishaji wa Brendan Rodgers, nilimjua kitambo.

“Anapenda kucheza soka la pasi na la kuvutia na mimi binafsi ninapenda makocha wanaopenda kushambulia.

“Naamini matokeo ya Alaves hayawezi kuathiri mchezo wetu wa leo.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV