September 13, 2016

Baada ya kuibuka kwa malalamiko kadhaa juu ya nyasi za Uwanja wa Uhuru kuwa hazina ubora mzuri kuweza kutumika na zimekuwa zikichangia kuwaumiza wachezaji, Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limetolewa ufafanuzi suala hilo.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas ndiye ambaye amelifafanua suala hilo wakati alipoulizwa, alidai kuwa uwanja una ubora na utaendelea kutumika.


 Wachezaji kadhaa wa timu ambazo zimeshautumia uwanja huo walilalamika kuwa kuna ubora unakosekana kwenye nyasi hizo wakiwemo Laudit Mavugo wa Simba na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambao walisema kuwa wanahitaji muda kuuzoea uwanja huo kwa kuwa nyasi zake hazina ubora mzuri kama zilivyo zile za Uwanja wa Taifa.

Mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars ambaye pia ni mchambuzi wa soka katika Gazeti la Championi aliiambia SALEHJEMBE kuwa licha ya kuwa yeye hajacheza kwenye uwanja huo wa Uhuru lakini anahisi nyasi hazina ubora kwa kuwa hata mpira unavyodunda tu inaonyesha kabisa hauna ubora mzuri.

Alfred Lucas amenukuliwa akisema: “Nyasi ni nzuri na hata kama mvua ilivyesha maji yakatuama na kudaiwa kuwa yalichangia mchezo kukosa ubora, siyo sahihi kwa kuwa uwanjani kuna mwmauzi ambaye naye anaona kinachoendelea kw aukaribu zaidi kama kuna tatizo basi yeye anatakiwa kuwa mtu wa kwanza kubaini hilo, lakini kwa kuwa aliruhusu mchezo ukaendelea na inaonyesha hakukuwa na tatizo kubwa.

“Watu wasitafute visingizio kwa hoja nyepesi, nafikiri hilo linatakiwa kueleweka.”

Aidha, Lucas aliongeza kuwa hakutakuwa na mabadiliko ya ratiba kwa ajili ya mchezo wa Simba dhidi ya Azam FC ambao utachezwa hapohapo kwenye Uwanja wa Uhuru, Jumamosi ijayo.

“Taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mchezo huo umebadilishwa ratiba siyo kweli utachezwa hapohapo kwa kuwa tathimini iliyofanyika inaonyesha kuwa uwanja huo unaingiza watu 22,000, hivyo unaweza ku-afford mchezo huo,” alisema Alfred.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV