September 4, 2016
Na Saleh Ally 
KOCHA Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger, ametabiri kwamba si muda mrefu sana kuna klabu itamwaga pauni milioni 200 (Sh bilioni 565) kumnunua mchezaji kutoka klabu moja kwenda nyingine.

Wenger kama ilivyo kawaida yake, anapinga hali hiyo, hasa baada ya Manchester United kukubali kumwaga pauni milioni 100 (zaidi ya Sh bilioni 282) kumpata Paul Pogba kutoka Juventus, mchezaji ambaye ilimuuza kwa bei chee kwenda kwenye klabu hiyo.

Ukiangalia manunuzi ya Pogba, ndani ya kipindi cha miaka michache tu, inaonekana dau la manunuzi ya wachezaji kutoka klabu moja kwenda nyingine hasa kwa ligi moja kwenda nyingine, limepanda kwa wastani wa pauni milioni 75 (Sh bilioni 212).

Kwani hata Wenger aliyeonekana ni mbahili sana, alimwaga zaidi ya pauni milioni 40 (Sh bilioni 113) ili kumnasa Mesut Ozil kutoka Real Madrid.

Soko la Ulaya sasa limetawaliwa na vitengo viwili tu. Moja ni biashara ya manunuzi ya wachezaji England na pili ni Ulaya nzima unaweza kuijumlisha ili kupata soko moja.
Wenger ameona soko la England lina hatari kubwa, licha ya kwamba yeye anaonekana mbahili lakini anaamini klabu zote zinazonunua wachezaji kwa bei ya juu zimekuwa zinajifunga bila ya zenyewe kujua.


Wenger ametoa sababu mbili katika hilo; moja ni klabu hizo kujikuta zikilazimika kubaki na wachezaji haohao. Hata kama hawatafanya vizuri zinashindwa kuwauza kwa bei ya chini kwa kuwa ziliwanunua kwa bei ya juu.

Kibiashara inakuwa tatizo lakini inakuwa tatizo pia kwa kocha ambaye angependa mchezaji huyo kama hafanyi vizuri aende na kupata mwingine ampe nafasi hiyo.


Pili; Wenger anaamini kama klabu haimuuzi, hulazimika kumpeleka mchezaji kwa mkopo katika klabu nyingine, mfano iwe nje ya England au klabu nyingine zisizoweza kulipa. Hapo klabu hiyo itamuachia mchezaji na kujikuta inaendelea kumlipa mshahara.

Hali kama hii, iliwatokea Tottenham Hotspur kwa Emmanuel Adebayor na jambo hili limekuwa likiendelea kuzitokea klabu za England ambazo nyingi zina wachezaji watano hadi 10 ambazo zinaendelea kuwalipa mishahara mikubwa ili mikataba yao iishe tu halafu waende.

Wenger anakiri kwamba kutokana na mkumbo huo wa klabu kubwa kutumia fedha nyingi, Arsenal inajikuta inachotwa na mwisho kulazimika kuingia kwenye mfumo wa kutumia fedha nyingi.

Kwani katika dirisha lililopita, Wenger amejikuta akilazimika kumwaga dola milioni 167 (zaidi ya Sh bilioni 357), hivyo kuwa moja ya klabu zilizotumia fedha nyingi. Manchester City ndiyo imeongoza kwa kutumia dola milioni 315.

Hata hivyo, Wenger anaendelea kusisitiza, hata kama ni ubora wa uwanjani, klabu ya soka lazima inaponunua iwe na hesabu katika uuzaji na Manchester United pamoja na Manchester City anaziona ni klabu zinazofanya mambo yao kwa kubahatisha, hasa unapozungumzia biashara.


Kwa nini anaziona zinabahatisha? Kocha Jose Mourinho alipotua tu akaanza kuponda mamilioni kwa kununua wachezaji kwa zaidi ya dola milioni 200 au pauni milioni 100 na ushee. Licha ya Pogba, aliwanunua Henrikh Mkhitaryan (kwa pauni milioni 37) na Eric Bailly (pauni milioni 33),  huku Zlatan Ibrahimovic akinunuliwa kama mchezaji huru. Wenger anatabiri, Man United itaendelea kupata hasara tu, linapofikia suala la kuuza.

Kumbuka kipindi chote wakati wa Louis van Gaal, United walitumia dola milioni 215 katika manunuzi, Man City chini ya Manuel Pellegrini wakatumia dola milioni 310. Klabu hizo za Jiji la Manchester zikapata hasara katika uuzaji.

 Mfano City waliuza kwa kiasi cha dola milioni 29 pekee, hasara yao ikawa dola milioni 285 na United wakauza kwa kipindi cha dola milioni 8 tu, hasara ni dola milioni 264. Hili ndilo Wenger hataki kulisikia.

Kuhusu takwimu, zinaonyesha dola bilioni 1.79 zimetumika kwenye usajili wa Ligi Kuu England katika dirisha lililofungwa juzi na kufanya ivunje rekodi ya usajili katika dirisha la msimu uliopita ambalo lilitumia dola bilioni 1.5 ambazo ni pauni milioni 870.

Kwa mara ya kwanza, unaona Wenger anaweka hadharani hofu yake ingawa amekuwa akionekana ni mbahili.


Lakini inaonekana hivi; timu zinazotoa fedha nyingi, pia huingiza faida kwa njia nyingine kama uuzaji wa jezi, mechi zao kujaza sana watu, kupata haki kubwa za malipo ya runinga. Hii inasababishwa na mashabiki pia kuvutiwa na wachezaji wapya. Sasa wewe unaweza kuangalia mjadala huu kama Wenger yu sahihi, au wengine ndiyo wako sahihi!


 FEDHA AMBAZO KLABU ZIMEMWAGA KIPINDI CHA USAJILI EPL 2016-17 (Kiwango ni kwa dola milioni)

1. Manchester City - 315m

2. Manchester United – 272m

3. Arsenal – 167m

4. Liverpool FC – 118m

5. Chelsea FC – 118m

6. Watford – 108m

7. West Ham United – 92m

8. Crystal Palace – 87m

9. Everton FC – 78m

10. Leicester City – 70m

11. Southampton – 69m

12. AFC Bournemouth – 55m

13. Tottenham Hotspur – 54m

14. Swansea City – 47m

15. Middlesbrough – 37m

16. West Brom – 32m

17. Stoke City – 31m

18. Sunderland – 24m

19. Burnley – 19m


20. Hull – 8m

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV