September 19, 2016

Kiungo mkabaji wa Yanga, Mzimbabwe, Thabani Kamusoko juzi Jumamosi aliugua ghafla ugonjwa wa kiungulia na kushindwa kumaliza mechi dhidi ya Mwadui FC.

Yanga ilivaana na Mwadui kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyomalizika kwa timu hiyo kushinda mabao 2-0 yakifungwa na Amissi Tambwe na Donald Ngoma.

Kamusoko (kushoto) akiwa na Kessy na Ngoma.

Yanga hivi sasa ina pointi 10 ikicheza michezo minne huku Simba ikiongoza ikiwa na pointi 13 baada ya juzi Jumamosi kuwafunga Azam FC bao 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.


Akizungumza na Championi Jumatatu, daktari mkuu wa timu hiyo, Edward Bavu, alisema kiungo huyo alishindwa kumalizia mechi na Mwadui baada ya kupata kiungulia ghafla katikati ya mchezo huo.


Bavu alisema wamegundua tatizo baada ya kumfanyia vipimo, hivyo tayari amempatia matibabu na hivi sasa anaendelea vizuri na mechi ijayo dhidi ya Stand United atakuwepo uwanjani.


Aliongeza kuwa, beki wao wa kati raia wa Togo, Vincent Bossou, amepona malaria na anaendelea vizuri baada ya kumpatia matibabu, naye mechi ijayo atakuwepo kama kocha akihitaji kumtumia.


"Kamusoko anaendelea vizuri, mechi ya jana (juzi) alishindwa kuendelea na mechi katika kipindi cha kwanza baada ya kuugua ghafla kiungulia.


"Alikuwa ana uwezo wa kuendelea mechi na Mwadui, lakini nikashauri kumpumzisha kwa hofu ya kiafya baadaye lisije likatokea tatizo kubwa.


"Kwa sababu tatizo hilo alilolipata wakati mwingine linatokana na tatizo la moyo na chakula ambacho mchezaji amekula, hivyo nikashauri tumtoe kwa ajili ya vipimo zaidi," alisema Bavu.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic