September 19, 2016



Azam FC ni kati ya timu bora za Tanzania Bara katika kipindi cha misimu minne iliyopita. Lakini bado kwa msimu huu ndani ya mechi tano unaweza kuiita kwa jina hilohilo.

Tunajua katika kipindi hicho imepitiwa na makocha kadhaa, mfano Stewart Hall raia wa Uingereza, Joseph Omog kutoka Cameroon ambaye sasa yuko Simba na kadhalika.

Lakini utaona ubora wa Azam FC katika kipindi hicho unadhihirishwa na takwimu na si maneno kwa kuwa kama haikuwa bingwa, basi ilishika nafasi ya pili.

Mwendo wa Azam FC katika kipindi hicho, umevuruga kabisa hali ya mazoea kwamba wakubwa kisoka katika nchi hii ni wawili tu, Yanga au watani wao Simba.

Wakongwe hao walikuwa wakipeana pasi za ubingwa, kama si huyu basi ni yule. Hata katika nafasi mbili za michuano ya kimataifa ni suala la kuangalia nani achue nafasi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya au Kombe la Shirikisho.

Lakini unaona kipindi chote hicho, Azam FC imekuwa mshiriki huku mkongwe mmoja Simba anaonekana kudorora na kuwapa mashabiki wake hasira na hamu kuu ya kurejesha heshima yao ya enzi, bado wanapambana.

Msemaji wa Azam FC, Jaffar Iddi Maganga aliwaudhi mno mashabiki wa Simba, hii ilitokea siku tatu aliposema Azam FC ni timu bora kuliko Simba kwa misimu ipatayo mitatu, minne. Hakuna haja ya kukasirika kwa kuwa alichokuwa akisema ni ukweli.

Kwa maana ya ukubwa wa historia na rekodi, Simba ni kubwa sana kwa Azam FC. Lakini kitakwimu kwa misimu hiyo mitatu, minne. Azam FC kweli ni bora zaidi ya Simba.

Sasa Azam FC ina makocha kutoka Hispania, makocha wote ni vijana ambao kama utahudhuria mazoezi yao, hakika utaona ni watu ambao wanataka mafanikio na kuna jambo wanalijenga ndani ya kikosi hicho.

Mazoezi yao ni makali lakini utaona namna ambavyo vijana wa Azam FC wanavyoyafurahia. Utaona sura za umoja na wachezaji wanavyoonekana wako tayari kufanya vema kwa ajili ya klabu, wao wenyewe na timu yao.

Zeben Hernandez ndiye kocha mkuu ambaye na kikosi chake ambacho kina kocha msaidizi, kocha wa viungo, daktari na mtaalamu wa masuala ya upishi. Hakika ni watu wanaojituma na huenda uongozi wa Azam FC unapaswa kupongezwa kwa kuwa na mipango ya kufanya mambo kwa weledi zaidi.

 Wahispania hao, wameingoza Azam FC kucheza mechi tano za ligi na hadi sasa wana pointi 10. Hii ni baada ya kushinda tatu, sare moja na kupoteza moja dhidi ya Simba, juzi.

 Baada ya kupoteza mechi moja dhidi ya Simba, kumekuwa na mijadala mingi huku watu wakiamini uwepo wa Wahispania hao kama hakuna lolote. Jambo ambalo si sahihi na Azam FC wanapaswa kuwa nalo makini.

Zeben na wenzake wanajaribu kuingiza mfumo mpya ndani ya kikosi cha Azam FC. Kamwe haliwezi kuwa suala la siku mbili au tatu, lazima kutakuwa na hatua pamoja na kukwama.

 Kutengeneza na kuujaza mfumo mpya katika mchezo wa soka, si jambo la wiki moja au mbili. Muda unahitajika na lazima mabadiliko yapatikane kwa kucheza. Timu hujengwa huku ikicheza, makosa yakipatikana yanafanyiwa kazi kwa vitendo na mwisho kurekebika.

 Haiwezekani ifundishwe darasani halafu ishinde tu uwanjani. Wala haitakuwa sahihi hata kidogo kuanza kuhoji kwamba kwa kuwa ni Wahispania, vipi timu haijashinda. Badala yake iangaliwe muda walioingia, upya wa kikosi katika sehemu kadhaa na mambo mengine.


 Lakini Azam FC kufungwa na Simba iliyoimarika pia isionekane ni dhambi. Uongozi wa Azam FC pia unapaswa kuwa makini na maneno ya kishabiki ambayo kama watayageuza kuwa ndiyo uamuzi wao, basi mwisho watajichanganya wenyewe.

Muda hauonyeshi kama Zeben na wenzake kuwa wameshindwa, badala yake hata mechi dhidi ya Yanga, walionyesha wanaweza kupambana, wakashinda mechi ya Ngao ya Jamii, pia dhidi ya Simba pamoja na kushindwa walionyesha wana kikosi bora.


Hivyo maneno ya mitaani yasije yakauzidi nguvu ukweli, mwisho Azam FC itajichanganya na kugundua ilikosea, baadaye wakati ikiwa haina uwezo wa kurudi nyumba. Hao Wahispania, wapewe nafasi ili tujifunze kutoka kwao.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic