September 9, 2016

Baada ya juzi Jumatano, Uwanja wa Uhuru uliopo jijini Dar es Salaam kuanza kutumika kwa mechi za Ligi Kuu Bara, rekodi tano zimewekwa uwanjani hapo kwenye mchezo kati ya Simba na Ruvu Shooting.

Uwanja huo ambao ulikuwa kwenye marekebisho yaliyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu, utakuwa ukitumika kwa baadhi ya mechi za ligi kuu na Ligi Daraja la Kwanza.

Uwanja wa Uhuru

Katika mchezo huo ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Ibrahim Ajib na Laudit Mavugo huku lile la Ruvu likifungwa na Abrahman Mussa, Ruvu imeweka rekodi tatu huku Simba ikiweka mbili.


Kadi ya kwanza ya njano/nyekundu
Ajib alikuwa mchezaji wa kwanza kuonyeshwa kadi ya njano katika dakika ya saba baada ya kuanguka kwenye eneo la hatari la Ruvu, lakini mwamuzi, Ngole Mwangole akamzawadia kadi hiyo kwa kile kilichoonekana kujaribu kumdanganya. Mbali na kadi hiyo ya njano, mchezo mzima ulikuwa na kadi tisa za njano na moja nyekundu.

Kiungo wa Ruvu, Jabir Aziz ‘Stima’ alitolewa uwanjani kwa kadi nyekundu kufuatia kumchezea vibaya kiungo wa Simba, Mzamiru Yasin katika dakika ya 80. Hakuonyeshwa kadi nyekundu moja kwa moja, bali kabla ya kufanya madhambi alikuwa na kadi ya njano, ndipo mwamuzi akamuonyesha nyingine ya njano iliyofuatia na nyekundu.

Bao la kwanza
Mchezo mzima ulikuwa na jumla ya mabao matatu. Ruvu ndiyo walikuwa wa kwanza kuziona nyavu za uwanja huo katika dakika ya nane kupitia kwa Abrahman Mussa aliyepiga shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari la Simba.

Ushindi wa kwanza / kipigo cha kwanza
Haitatokea tena timu nyingine kuwa na rekodi hizi kwani tayari rekodi ya kushinda imeshachukuliwa na Simba huku ile ya kufungwa wanayo Ruvu. Rekodi pekee iliyobaki ni kwa timu kutoka sare.

Baada ya kushinda mchezo huo, Simba imejikusanyia pointi saba sawa na Azam na Mbeya City lakini yenyewe inashika nafasi ya tatu baada ya kuzidiwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Azam ya kwanza ikifuatiwa na Mbeya City.SOURCE: CHAMPIONI0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV