September 19, 2016

Kufuatia kufunga bao pekee katika mchezo wa juzi Jumamosi dhidi ya Azam FC, kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya ametuma salamu akisema anaisubiri Yanga.

Kichuya ambaye sasa ni mmoja wa wachezaji wanaopendwa na mashabiki wa Simba, ametamba kuwa wapo tayari kucheza na  Yanga wakati wowote kuanzia sasa kutokana na ubora wa kikosi chao na kamwe hawawezi kuwahofia.

Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Oktoba Mosi katika mchezo ambao umeshavuta hisia za wengi. Timu zote zipo kwenye ubora wa aina yake, Yanga waliwafunga Mwadui mabao 2-0 wakiwa ugenini kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, juzi.  



Simba iliifunga timu ngumu zaidi ya Azam FC bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, huku Kichuya akifunga bao hilo pekee kwa ustadi mkubwa na kupanda kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiw ana pointi 13.

Kichuya aliyejiunga na Simba akitokea Mtibwa Sugar kwa mkataba wa miaka miwili, amefanikiwa kucheza michezo yote mitano akiwa na kikosi cha Simba na kufanikiwa kufunga mabao mawili mpaka sasa.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Kichuya alisema kuwa hawawezi kuwahofia Yanga hata kidogo na wapo tayari kucheza nao wakati wowote kwani amekuwa akimuomba Mungu amuongoze kufunga mabao katika kila mchezo anaocheza.


“Unajua nimekuwa nikijituma kila siku ili niweze kufunga mabao, sasa nashukuru nimeweza kufunga kwa sababu nimekuwa nikimuomba kila siku niwe nafunga kitu ambacho kimetokea leo (juzi) maana ukiangalia Azam ndio walikuwa wapinzani wetu lakini kwa kuwa tumewafunga sisi ndio tunaongoza ligi.


“Kilichobaki kwetu ni kuendelea kupambana kwa sababu suala la kupata ubingwa lipo wazi kabisa kutokana na kikosi ambacho tunacho, mechi bado nyingi sana, tunajua baada ya kucheza na Majimaji tutacheza na Yanga lakini hatuwezi kuwahofia, waje tu, maana tupo tayari kwa lolote,” alisema Kichuya.


Kichuya aliongeza kuwa tangu walipoanza kuutumia Uwanja wa Uhuru kwa mechi za Ligi Kuu Bara, kuna ahadi aliiweka moyoni ambayo juzi Jumamosi aliitimiza.


Kichuya alipofunga bao alikwenda moja kwa moja kwenye bango lililokuwa kusini mwa uwanja huo likiwa na picha ya kiungo wa zamani wa Simba, Patrick Mafisango na kupiga saluti.


Ameliambia gazeti hili kuwa, Mafisango alipokuwa akiichezea Simba, alikuwa ni mchezaji anayempenda zaidi na ndiyo maana juzi akamuenzi kwa staili hiyo.


“Kila siku nilikuwa naliona lile bango likiwa na picha ya Mafisango, nikasema endapo siku nikifunga bao basi lazima niende kushangilia pale.


“Kama uliniona nilipofunga nilitaka kwenda kushangilia walipokuwa mashabiki, lakini nilipokumbuka ile ahadi yangu, moja kwa moja nikaenda lilipo lile bango ambalo nilikuwa naliona kila siku, nikapiga saluti, watu wengi wanadhani nimewapigia saluti mashabiki, kumbe nilimpigia Mafisango ambaye kiukweli nilikuwa nampenda sana,” alisema Kichuya.


Ikumbukwe kuwa, Mafisango ambaye alikuwa raia wa Rwanda mwenye asili ya DR Congo, alifariki dunia Mei 17, 2012 kwa ajali ya gari akiwa jijini Dar. Kiungo huyo alijiunga na Simba mwaka 2011 akitokea Azam FC.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic