September 30, 2016Simba wametua jijini Dar es Salaam kimya kimya, jana. Halafu leo wakafanya mazoezi kwa muda mfupi tu kwenye Uwanja wa Gymkhana.

Mazoezi ya Simba, yalionekana ni ya kupasha moto misuli tu na huenda yakawa ndiyo ya mwisho, yaani jioni watakuwa wamepumzika tu.

Lakini watani wao Yanga, wanatarajia kurejea Dar es Salaam leo, wakitokea mjini Pemba ambako pia wameweka kambi.

Hii ni sehemu ya joto la mechi ya watani ambayo itapigwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Leo wa Yanga wanaendeleza ule msemo wa kuwa wao ni wa kimataifa kwa kupiga masafa anga kwa anga, hiyo ni baada ya kuamua kukodisha ndege maalum kutoka Pemba kuelekea Dar es Salaam kuwavaa watani wao wa jadi, Simba, kesho Jumamosi.


Ishu ipo hivi, Yanga walitoka Shinyanga, Jumatatu ya wiki hii wakitoka kuvaana na Stand United, wakapanda ndege kurejea Dar es Salaam, kisha wakaunganisha kwenda Pemba kwa ndege kuweka kambi kwa ajili ya mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara.

Taarifa zinaeleza ni kuwa Yanga imepanga kurejea Dar, leo Ijumaa jioni mara baada ya mazoezi asubuhi watakayofanya kwenye Uwanja wa Gombani na kurejea hotelini kupumzika kisha jioni kupanda ndege hiyo.

"Hatutaki kuona wachezaji wetu wakipata uchovu wa safari na ndiyo sababu ya sisi kutumia ndege katika safari zetu, kama unakumbuka tulienda Shinyanga na ndege, tukarudi Dar na ndege kabla ya kubadilisha nyingine kuelekea Pemba.


"Timu yetu ipo vizuri, tunashukuru kikosi chetu kipo fiti kwa maana ya kutokuwa na majeruhi kwa wale waliokuwepo," alisema mtoa taarifa huyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV