September 12, 2016

Miongoni mwa Waafrika walioamua kuweka elimu pembeni na kupambana na soka kuwa maisha yao, Samuel Eto’o ni mmoja wao. Siyo kwamba hana elimu kabisa, anayo lakini akiwa na umri mdogo wa chini ya miaka 18 aliamua kwenda Ulaya kutafuta maisha.

Wakati akizunguka huku na huko kutafuta maendeleo yake ya soka, Eto’o alikutana na mitihani mingi lakini hatimaye alifanikiwa kutoboa na kuwa staa, kikubwa zaidi ni kuwa alifanikiwa kuwa mchezaji tajiri.

Eto’o, Georgette siku ya ndoa yao.
 
Kuna kipindi Eto’o, 35, alishawahi kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa kuliko wote akiwazidi hata Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, wakati huo alipokuwa akiichezea Anzhi Makhachkala ya Urusi.

Historia inaonyesha kuwa mchezaji huyo raia wa Cameroon, alitua Hispania kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa ndani ya Real Madrid, alipotua kwenye uwanja wa ndege uliopo Madrid, akalazimika kusubiri kwa saa tisa ili wenyeji wake watokee kumchukua.

Hiyo ilikuwa mwaka 1997, akafanikiwa na kujiunga katika timu ya Real Madrid B, baadaye timu hiyo ikashushwa daraja hadi daraja la tatu ambapo wachezaji wasio raia wa nchi za Ulaya hawakuruhusiwa kucheza, ikabidi apelekwe kwa mkopo katika timu ya Leganés iliyokuwa daraja la pili. Ilikuwa msimu wa 1997/98.

Aliporejea Madrid, akatolewa kwa mkopo kwenda Espanyol, akashindwa kucheza hata mechi moja , aliporejea Madrid akatolewa tena kwa mkopo Real Mallorca iliyokuwa ikishiriki La Liga, akaonyesha uwezo mzuri na timu hiyo ikamsajili moja kwa moja kwa pauni milioni 4.4.

Hasira alizokuwa nazo za kutafuta mafanikio na kutopewa thamani ndani ya Madrid, akapambana kwa nguvu kwa kuwa alijua akifeli basi ameifelisha hata familia yake iliyobaki Afrika.

Uwezo mkubwa aliouonyesha hapo ukasababisha Barcelona watoe dau la euro milioni 24 kumsajili, Madrid walipotaka kukwamisha dili hilo ili wamnunue wao tena, ikashindikana. Alipotua Barcelona kilichofuata ni historia.

Wakati akiendelea kupata mafanikio hayo na dunia nzima ikitambua kuwa Mcameroon huyo aliyeweka rekodi nyingi Ulaya na Afrika katika michuano mbalimbali, naye ana historia yake ya nyuma ya pazia kuhusu maisha ya kimapenzi.


Eto’o, Georgette siku ya ndoa yao.


Eto’o ambaye kwa sasa anaichezea Antalyaspor ya Uturuki, akiwa ni kocha mchezaji, anasimulia: “Nilikutana na mke wangu (Georgette Tra Lou) wakati huo nilikuwa bado chipukizi, nilikuwa nacheza soka la mtaani nchini Ufaransa.

“Kuna siku nilienda kuomba kujiunga katika timu ya FC Nantes ya Ufaransa, wakakataa kunichukua lakini yeye (mpenzi wake ambaye sasa ni mkewe) alikuwa na imani nami, akanipa moyo wa kupambana na kutokata tamaa.

“Nilikuwa sina kitu, yeye ndiye aliyekuwa akihusika na masuala mengi ya kunigharamia. Alikuwa akimiliki saluni maeneo ya Nantes.

“Alinivumilia kwa mengi na kunipa moyo wa kujituma, leo hii Georgette ni mke wa mchezaji tajiri Afrika, kwa pamoja tuna zaidi ya euro milioni 100 katika akaunti zetu, nina furahi kumuoa mwanamke mvumilivu.”
Hii ndiyo simu aliyokuwa akiitumia Eto’o enzi zake.Wakati huo Eto’o alikuwa akimiliki simu aina ya Nokia 3310, ambayo kwa mpenzi wake huyo raia wa Ivory Coast, aliona kama ‘sweet’ wake anamiliki simu ya bei kubwa, leo hii Eto’o anamiliki kampuni yake ya simu.

Baada ya kuwa kwenye uhusiano wa muda mrefu wa mtu na mpenzi wake huku Eto’o akipambana katika timu tofauti kwenye soka, hatimaye mapema mwaka huu walifanikiwa kufunga ndoa ya kanisani baada ya awali kuripotiwa kufunga ndoa ya kienyeji.

Ndoa hiyo ya kanisani ilifungwa nchini Italia na kuhudhuriwa na wachezaji kadhaa akiwemo nahodha wa zamani wa Barcelona, Carles Puyol.

Ukiachana na timu ya taifa ya Cameroon ambayo aliichezea mechi 118 na kufunga mabao 56 kuanzia mwaka 1997 hadi  2014, Eto’o pia alicheza soka katika klabu za Inter Milan, Chelsea, Everton na Sampdoria.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV