September 20, 2016


Wabunge wapenzi wa Simba wanatarajia kuumana wikiendi hii, ikiwa ni mechi mahsusi kwa ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia wahanga wa tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibuni huko mkoani Kagera.

Mbali na mechi hiyo pia kutakuwa na mechi za ufunguzi baina ya Bongo Muvi dhidi ya Bongo Fleva, pia kutakuwa na mechi ya netiboli itakayoikutanisha timu ya bunge dhidi ya ile ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), mechi zote hizo zitapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Mbunge wa Sengerema na Mwenyekiti wa Bunge SC, William Ngeleja ameweka wazi kuwa licha ya wabunge hao kuchangia kiasi cha Sh milioni 85 kupitia posho zao wakiwa bungeni lakini bado wameona kuna msaada zaidi unahitajika kwa ajili ya angalau kurejesha hali ya maisha ya awali ya Kagera ndiyo maana kumeandaliwa mechi hizo.

“Lengo letu ni kukusanya fedha za kuwasaidia ndugu zetu wa kule Kagera, angalau warejewe na hali waliyokuwa nayo awali, tangu awali kule bungeni kupitia posho zetu tulishachanga milioni 85 lakini tunahitaji kuongeza zaidi misaada kwao ndiyo maana tumeandaa mechi hii ili kila Mtanzania kupitia kiingilio alichonacho naye ashiriki kuwakomboa ndugu zetu hawa.

“Vikosi vitakuwa vikali kwa ajili ya kutoa burudani ya kutosha, huku kwetu Simba tutakuwa na Kassim Majaliwa, Hamis Kigwangwala, Kaizer Makame na wengine. Kule Yanga nao watakuwa na Ridhiwani Kikwete, Anthony Mavunde, Mwigulu Nchemba na wengine wengi.

“Bongo Muvi wao watakuwa na kina Ray Kigosi, JB, Muhogo Mchungu, Dk. Cheni na wengine, lakini Bongo Fleva wao watakuwa na kina Tundaman, Ali Kiba, Diamond, KR Mullah na wengine. Kuhusu mgeni rasmi, tunakamilisha taratibu na muda si mrefu tutamtangaza,” alisema Ngeleja ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Sengerema.

Tayari viingilio vya mechi hiyo itakayopigwa Jumapili hii vimeshawekwa wazi ambapo Sh 3,000 itakuwa kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, Sh 10,000 na 15,000 itakuwa kwa ajili ya viti vya rangi ya machungwa huku Sh 50,000, 100,000 na 200,000 ikiwa ni kwa V.I.P C, B na A.

Lakini kwa viti 50 pekee maalum vitakavyokuwa karibu na mgeni rasmi wa mechi hiyo ambaye atatajwa baadaye, kila kimoja kitalilipiwa Sh 1,000,000.

  

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV