Beki wa kati wa Azam FC, Aggrey Morris, amemvunja taya mshambuliaji wa Stand United raia wa Nigeria, Abasrim Chidiebere, baada ya kumpiga kichwa.
Tukio hilo, lilitokea wakati timu hizo zilipovaana juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliomalizika kwa Stand kushinda bao 1-0.
Kocha Msaidizi wa Stand, Athumani Bilali ‘Bilo’, alisema Chidiebere alipoteza fahamu kwa saa sita kuanzia saa 10:20 jioni hadi 4:00 usiku baada ya kupigwa kichwa na Morris wakati wa mechi hiyo.
“Alizimia palepale, akawa anatoa damu nyingi mdomoni na puani, aliokolewa na madaktari walioingia uwanjani na kisha kumchukua kumpeleka kwenye gari la kubebea wagonjwa lililompeleka hospitali.
“Baada ya vipimo ilibainika kuwa alivunjika taya zote. Ni jambo la kushukuru Mungu, pia tunawashukuru viongozi na benchi la ufundi la Azam waliofika hospitalini leo (jana) asubuhi kwa ajili ya kumjulia hali yake,” alisema Bilo.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment