Na Saleh Ally
NIMEKUWA wazi mara nyingi sana kuhusiana na Kocha Jamhuri Kihwelo maarufu kama Julio. Kwamba ni mmoja wa ninaowakubali hasa unapozungumzia makocha wazalendo.
Nimeeleza mengi na kuwakumbusha ambao wamekuwa wakimbeza. Kwamba Julio ni mmoja wa makocha bora kabisa wazalendo ndani ya nchi zao, hapa Tanzania, wote tunalijua hili, yeye ni mmoja wa walio bora kabisa.
Nimekuwa nikikumbushia uwezo wake na achana na wakati akiinoa Simba. Aliipandisha Mwadui FC misimu miwili iliyopita, lakini zikapita figisu, nafasi yao ikaenda kwa Stand United. Pamoja na kulalamika, aliahidi msimu unaofuata, lazima Mwadui FC ipande, kweli tuliona, ikapanda, huku ikichukua ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
Kweli ikarejea Ligi Kuu Bara baada ya miaka zaidi ya 20, Mwadui FC ikawa moja ya timu chache tishio kwa vigogo. Hii ni sehemu ya kuthibitisha ubora wa Julio ambaye aliwahi kutamba na timu ya Dar es Salaam ‘Mzizima United’ na hata timu za vijana.
Pamoja na hivyo, hivi karibuni alianza kutangaza kuhusiana na nia yake ya kutaka kuachia ngazi kwa kuwa amechoshwa na uonevu. Julio amelalamika hadi amefikia uamuzi huo wa kujiuzulu kuinoa Mwadui FC.
Sababu kuu ya Julio ni kukaa mbali na uonevu wa waamuzi ambao anaamini wamekuwa wakifanya hivyo kwa maslahi yao binafsi.
Uongozi wa Mwadui FC, mwisho umeridhia na kusema umemkubalia Julio kuondoka ingawa pia umefanikiwa ‘kumpata’ kama mshauri wao. Awali, niliona kama anatania, mwisho akafikia uamuzi wake, kweli nimeshangazwa sana.
Uamuzi wa Julio kujiuzulu baada ya kuchoshwa na uonevu wa waamuzi, kwanza, nikubaliane na Julio kwamba waamuzi wa Tanzania, wengi wana matatizo tena mengi ambayo yanatia unyonge na kichefuchefu.
Ninaamini kuna waamuzi wengi ambao si waaminifu na wanafanya hivyo kwa ajili ya maslahi yao binafsi na si mpira wa Tanzania, jambo ambalo ni baya sana na adui mkubwa wa maendeleo ya soka nchini.
Hawa waamuzi hawaishi, hakika hawawezi kubadilika kwa wakati mmoja kwa kuwa hata wanaowaongoza, mfano Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), si wenye lengo hasa la kuendeleza na wametawaliwa au kuzungukwa na rundo la madudu na tunayaona.
Hawa waamuzi wataacha lini? Hatujui na kama Julio alisomea ukocha, tena baada ya kuwa mchezaji nyota na anajua kwa Mwadui FC yeye ni kamanda na alikuwa anastahili kuongoza jahazi, vipi akae kando eti fulani amefanya madudu au kundi fulani limeboronga?
Vipi hakuondoka baada ya Mwadui FC kunyimwa nafasi na Stand United ikashinda pointi na kupanda daraja? Kwani Julio hajui matatizo ya waamuzi tangu akiwa Kajumulo FC, baadaye Simba na kadhalika?
Hivi, hii ni mara ya kwanza Julio kutotendewa haki na waamuzi? Pia jiulize, kweli waamuzi wote waliwahi kutomtendea haki, hakuna ambao wamewahi kumtendea haki?
Julio aliyewahi kucheza kama mlinzi tegemeo wa Simba hadi kufikia kubandikwa jina la Mrema, kweli hajui kwamba Tanzania ina matatizo ya waamuzi! Na tujiulize kweli hatarudi tena kwa kuwa hatuna uhakika wa waamuzi hawa kubadilika kabisa na kufikia kiwango bora anachotaka Julio na sisi sote?
Kocha ni kama baba, kama jeshini ni kamanda, lakini wakiwa tayari wameingia kwenye uwanja wa vita, kamanda amevua gwanda kwa kisingizio cha kutotendewa haki! Ameamua kuwaacha vijana wake wapendwa wakipambana bila ya yeye.
Kweli yeye akiondoka Mwadui FC sasa watatendewa haki? Kama ni kiongozi sahihi vipi ameamua kuwaacha njiani? Kwangu namuona Julio ametafuta sababu ya kuondoka kutokana na sababu nyingine kwa kutumia sababu nyingine na inabidi ajipime kwa kuwa taratibu anaingia kwenye kundi la “Makamanda Waoga”.
0 COMMENTS:
Post a Comment