October 24, 2016


KALA ONGALA

Kocha Mkuu wa Majimaji, Kally Ongala, amefunguka kuwa kufanya vizuri kwa vijana wake kwa sasa ni kutokana na kila mmoja kujitambua na kuyafahamu majukumu yake ndani ya kikosi hicho.

Ongala ambaye amekabidhiwa timu hiyo hivi karibuni kutoka kwa kocha wa awali, Peter Mhina, tayari amefanikiwa kuiongoza kwenye mechi sita na kujikusanyia pointi 10.

Katika mechi hizo sita chini ya Ongala, wameshinda tatu, sare moja na kupoteza mbili ambapo kabla ya hapo, walikuwa wamecheza mechi sita na kufungwa zote, wakati huo kikosi hicho kilikuwa chini ya Mhina.

Ongala alikichukua kikosi hicho kikiwa mkiani, lakini kwa sasa kinashika nafasi ya tatu kutoka chini.

“Kwa sasa vijana wanapambana sana mazoezini, wanajitambua wanatakiwa kufanya nini, hali hiyo imechangia sana kupatikana kwa matokeo mazuri kwa sasa.

“Mbali na kujitambua kwao, lakini pia kuna ushirikiano mkubwa kikosini kwangu na kila siku zinavyosonga timu inazidi kukaa sawa kwa sababu kila mmoja anayafahamu majukumu yake ni nini na anayafanyia kazi kisawasawa, nadhani huko mbele tutazidi kuelewana vizuri zaidi.

“Bado tuna safari ndefu, tuna mechi nyingi muhimu ambazo ni lazima tupate pointi ili tuondoke kabisa huku maeneo ya mkiani mwa ligi,” alisema Ongala.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV