October 24, 2016





Na Saleh Ally
MAZUNGUMZO ya wapenda mpira wengi wa Tanzania huwa yamejaa lawama kutokana na mambo mawili makubwa.
Kwanza watu wengi hawapendi kujifunza mambo kabla ya kuanza kuyazungumzia au kuyaeleza na pili, wengi huamini kukosoa peke yake ndiyo jambo jema au kuonekana unajua sana.

Mfano, kama leo utaamua kusifia mazuri ya Shiza Kichuya, kuna mtu atakuuliza kwa nini haujazungumzia na mazuri ya Simon Msuva wa Yanga. Kwamba kila unapoizungumza Yanga, basi ni lazima Simba nayo izungumzwe.
Hii inajenga hisia za kutojifunza lolote la Yanga hadi Simba iwepo, jambo ambalo si sahihi na upotofu wa mawazo ambao huenda unawafanya watu wengi sana wasijifunze mambo mengi sana kwa kuwa wanataka kila kitu ‘wabalansi’.

Hakuna anayeangalia Simba inazungumziwa wakati gani na sababu ipi, pia Yanga inapaswa kuzungumziwa kwa jambo lipi na wakati gani. Nafikiri kuna kila sababu ya kufanya tafakuri jadidi na watu waanze kubadilika, la sivyo wengi tutabaki hohehahe kila tunapokuwa macho na angalau kila tunapopata usingizi.

Mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa alikuwa katika wakati mgumu sana kwa kuwa alinunuliwa na Yanga kwa kitita kikubwa cha fedha wakati akitokea FC Platinum ya Zimbabwe. Wakati anakuja, ndiye alikuwa tegemeo katika ushambuliaji wa kikosi cha Platinum baada ya kuwa kimeondokewa na Donald Ngoma ambaye pia amejiunga na Yanga.

Kweli hakuweza kufanya vizuri, huenda alipata bahati mbaya ya kuanza kuitumikia Yanga katika michuano migumu ya kimataifa. Aliikuta ikiwa imeanza kazi ya kucheza Kombe la Shirikisho hatua ya makundi, hatua ambayo hata Yanga haikuwa imeigusa miaka nenda rudi, kwake pia ilikuwa ni mara ya kwanza.

Mwenendo wake haukuwa mzuri na baada ya hapo, lawama kama ilivyo kawaida zikaanza na hakuna ambaye aliyetaka kujifunza na kuangalia kwamba Chirwa ana ugeni Yanga, ugeni huo unamfanya aanze kujifunza mengi ikiwa ni pamoja na kocha anataka nini na wachezaji wenzake wanachezaje.

Lakini hata mazingira kwa ujumla. Kila mmoja akawa anamsakama na ikafikia hata Katibu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali akamsema kuwa hana lolote, kauli ambayo hautegemei kuisikia kwa mzee wa klabu kama yeye! Maana yake inaukatisha tamaa uongozi, mchezaji mwenyewe na hata kuamsha maneno yasiyo na sababu za msingi.

Sijui tena kama mzee Akilimali anaweza kuinua mdomo na kusema kuhusiana na Chirwa! Wengine waliokuwa wakimsakama pia sijui wataficha wapi nyuso zao maana tayari ana mabao manne ndani ya mechi tatu alizocheza dakika 90 achana na zile alizokuwa akiingia kutokea benchi na inaonekana anaweza kufunga zaidi ya hapo.

Lakini hili lipo pia kwa washambuliaji wawili wa Simba, Laudit Mavugo na Frederic Blagnon. Hakika bado hawajashindwa na nafasi wanayo, lakini wako kwenye presha kwa kuwa kila mmoja anaona wao ni mizigo.
Hakuna anayeweza kuchambua kitaalamu kwa kuona wamecheza mechi ngapi, katika hizo mechi ni dakika ngapi kwa mchezo na zote walizocheza. Lakini pia, kwa nafasi waliyopewa wanaweza kutulia na kufanya vitu vya uhakika.

Kweli wana mtihani na kuufanya ni kazi yao, lakini bado wanaowatupia lawama nyingi wanapaswa kujifunza mambo mengi ya soka. Kumbuka mabeki nao huwapania zaidi kwa kuwa wangefurahi kuona wamewadhibiti.

Bado hata hao wawili, Blagnon na Mavugo ambaye jana amefunga tena, kama si wote, basi mmoja wao, atawashangaza watu kama ambavyo Chirwa alivyoanza kumshangaza mzee Akilimali na wengine waliokuwa hawamuamini.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic