October 24, 2016Juzi Jumamosi, Simon Msuva alifunga bao lake la 52 katika kikosi cha Yanga na baada ya mchezo akasema bao lake hilo amempa mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji kutokana na uongozi wake uliotukuka.

Msuva alikuwa kwenye ubora wa juu wakati Yanga ikiichapa Kagera mabao 6-2 katika Uwanja wa Kaitaba na licha ya kufunga bao hilo, alitoa pasi za mabao (asisti) mengine manne.

Mara baada ya mchezo huo, Msuva alisema kutokana na mwenyekiti wao Manji kuiongoza timu hiyo kwa mafanikio makubwa, basi anamzawadia bao lake hilo la 52.
 “Naushukuru uongozi wa timu yangu ya Yanga kwa kutuwezesha na kutusapoti lakini niseme kuwa bao langu la leo (juzi), nampa mwenyekiti wetu Manji iwe kama zawadi ya uongozi wake kwetu,” alisema.

Msuva amesema bado ana ndoto za kufunga mabao mengi kwa faida ya timu.
 “Bado ninahitaji kuvunja rekodi nyingi zaidi katika timu yangu, hivyo nitaendelea kujituma ili niweze kufanikiwa zaidi kupitia soka,” aliongeza.

Hadi sasa Msuva ana mabao manne msimu huu. Itakumbukwa kwamba aliwahi kuibuka mfungaji bora Bongo msimu wa 2014/15 baada ya kufunga mabao 17. Kwenye Kombe la Mapinduzi 2015 visiwani Zanzibar pia aliibuka mfungaji bora akifunga mabao manne.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV