October 7, 2016Na Saleh Ally
MECHI ya watani Yanga na Simba, huwa haiishi gumzo baada ya muda mfupi. Mara nyingi inakuwa na matukio ambayo yanazungumzwa kwa muda mrefu sana, hata baada ya kupita kwa mechi hiyo.

Gumzo kubwa baada ya mechi ya sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi iliyopita, ni suala la mwamuzi Martin Saanya ambaye hakika aliliboronga pambano hilo na hakuna anayeweza kumtetea.

Kuboronga kwake kunaanzia kukubali kwamba mshambuliaji Ibrahim Ajibu aliotea kabla ya kwenda kufunga katika dakika ya 6 tu. Lakini kuna mengi, aliachia faulo nyingi zifanyike kwa kuwa hakutoa adhabu.

Ubabe ulitawala, faulo mbaya za waziwazi zilitokea na hakuchukua hatua mapema kuwaonya na kuwaonyesha wachezaji wanapaswa kucheza soka na kuonyesha ladha ya soka na si ubabe au undava.

Waamuzi wa pembeni, wote walikuwa tatizo kubwa. Kwani mmoja anahusika kwenye kuruhusu bao lenye tatizo na mwingine kwenye kukataa bao sahihi. Huenda nao walichangia mwamuzi wa kati kuyumba zaidi.

Baada ya mechi na kwa kuwa ilikuwa ina madudu rundo, ile kamati ya Saa 72 ya Bodi ya Ligi ilikaa kwa ajili ya kupitia na kutoa uamuzi, mfano adhamu na kuondoa adhabu.

Mengi yamefanyika ikiwa ni pamoja na kutoa adhabu kwa Simba kutokana na vurugu za mashabiki wake, Msemaji wa Simba Haji Manara pia ameadhibiwa kwa kuingia uwanjani. Kama ni sheria kweli haliwezi kukwepeka kwa kuwa mambo yalikuwa wazi.
Lakini kuna ambayo yameshangaza na huenda katika kamati hiyo kulikuwa na watu walionuia kufanya jambo ambalo linaonyesha wazi ndani yake kuna ushabiki, maagizo au udogo wa ufahamu wa mambo.

Nahodha wa Simba, Jonas Mkude amefutiwa kadi yake nyekundu. Amefutiwa kwa madai inaonekana haikuwa halali, lakini hakuna maelezo ya kutosha kwa nini haikuwa halali.

Gumzo kubwa kwamba Mkude hakumsukuma mwamuzi Saanya. Watu wanajadili zaidi hilo, lakini nani ana uhakika Mkude hakusema lugha chafu au jambo ambalo si sahihi kwa mwamuzi? Kamati ilipata ripoti ya mwamuzi huyo? Jibu najua ni hapana, vipi imeamua madudu hayo!
Picha zinaonyesha hali ilivyokuwa.

Mkude anaonekana akimkimbilia Saanya akitaka kumvaa na wenzake wakimzuia. Tunaona wanavyozozana na hata ile clip ya video iliyokuwa ikijadiliwa kwenye runinga ni haraka tu, ukitulia utaona ndani yake kuna kosa linalohusiana na kinachokataliwa.

Kufutwa kwa kadi ya Mkude kunaweza kuwa makosa au ujanja kwa maana ya kukusudia. Lakini hii haimsaidii nahodha huyo wa Simba, angeweza kujifunza zaidi kwa kuwa kila aliyekuwa uwanjani aliona kwamba alishindwa kujidhibiti kama nahodha na kuwa kiongozi sahihi ambaye anapaswa kuwaongoza wenzake kwenye utulivu na si kwenda kwenye ugomvi.

Maana Mkude ndiye alikuwa akizuiwa na wengine, jambo ambalo si picha nzuri kwa nahodha. Kumfutia kadi ambayo sijui kama ililalamikwa na upatikanaji wake ulionekana wazi hauna kasoro, hakika si sahihi.
Kweli aliamua kufanya hivyo baada ya Saanya kufanya madudu yake. Lakini bado madudu ni madudu tu na sasa ni madudu mengine ya kuifuta yamefanyika.

Kamati hiyo pia, eti imechukua uamuzi wa kuendelea kufuatilia kuhusiana na uchezeshaji wa Saanya katika hiyo mechi, baadaye ndiyo itatangaza maamuzi.

Kitu kingine ambacho unaweza kukiita ni madudu ni hicho. Saanya na wenzake walitakiwa waangaliweje? Kamati ilikaa Jumanne, mechi ilichezwa Jumamosi. Kuiangalia mechi ni saa moja na nusu, ukiamua kuirudia tena itakuwa saa tatu. Kamati inaweza kukaa kwa saa mbili au tatu tena. Sasa nini kinachoangaliwa wakati kila kitu kipo?

Mimi naanza kupata hofu za wazi kwamba kamati hizi huendeshwa kwa maagizo ya watu fulani kwa ajili ya kuendeleza au kuvuruga mambo fulani, hii si kitu kizuri kwa afya ya soka la Tanzania na sifa bora ya udhaifu ndani ya mpira ambayo ni tetenasi kuu.


3 COMMENTS:

  1. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  2. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  3. Malizia tu kwahiyo wewe ulivyotaka Mkude aendelee na adhabu si ndio eenh?

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV