October 7, 2016


Katika kile kinachoonekana sasa presha imeanza kuwa kubwa kwa mabosi wa Ligi Kuu Bara kuhusu ubingwa, licha ya kuwa bado ni hatua za mwanzoni katika msimu wa 2016/17 tayari kumekuwa na tambo kila kona huku timu kubwa za Simba na Yanga zikianza kutupiana vijembe.

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm amewaambia wapinzani wake, Simba kuwa wanajidanganya kuufikiria ubingwa wa ligi hiyo kwa kuwa bado ni mapema.

Pluijm ametoa kauli hiyo mara baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga kumalizika kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 11 katika michezo sita huku Simba ikiwa inaongoza ligi ikiwa na pointi 17 katika mechi saba.

Pluijm amesema itakuwa ajabu Yanga kuondolewa kwenye mbio za ubingwa wakiwa wamecheza mechi sita tu.

"Kama wanajipa matumaini hayo ya ubingwa, basi watakuwa wanajidanganya, tungojee ligi imalizike halafu uone hao Simba kama watakuwa mabingwa," alisema Pluijm.

Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, amefunguka kuwa, mpaka sasa bado hajaona timu ambayo itakuja kuisumbua timu yake katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo.

“Najua si rahisi kuendelea kung’ang’ania kileleni wakati kuna mechi nyingi zimebaki, lakini hilo halitutishi sana, tutapambana iwe nyumbani au ugenini, ni lazima tupate pointi,” alisema Omog.


1 COMMENTS:

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV