November 19, 2016


Bosi wa benchi la ufundi la Simba, Joseph Omog, yupo kwao Cameroon kwa mapumziko lakini amewaambia viongozi wa timu yake kwamba hawatakiwi kukipangua kikosi ili kifanye vizuri baadaye.

Omog amewataka mabosi wake kutokitibua bila maelekezo yake kikosi chake kilichocheza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara badala yake wanatakiwa kukiongezea nguvu ili kifanye vizuri zaidi.

Hadi sasa Simba inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 35 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 33 huku timu zote zikiwa zimecheza mechi 15.

Akizungumza kabla ya kuondoka nchini, Omog alisema wakati huu wa usajili wa dirisha dogo, mabosi wake wanatakiwa kuyafanyia kazi mapendekezo yake aliyoyawasilisha kwenye ripoti na wasichukue uamuzi wa kuwatema wachezaji muhimu kikosini.

“Hatutakiwi kukiondoa kikosi hiki cha kwanza kwa namna yoyote ile kwa sababu kimetusaidia kufikia mafaniko haya, hivyo kumpoteza mchezaji yeyote yule aliyecheza katika mzunguko wa kwanza, litakuwa pigo kwa sababu ana umuhimu wake na bado wote nawahitaji katika kufanikisha kutwaa ubingwa.

“Cha muhimu wao wafanye kile ambacho tumekijadili kwenye ripoti kwa kuongeza mshambuliaji pamoja na mabeki wa kushoto na kulia kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi,” alisema Omog.

Tangu Novemba 15, mwaka huu timu za ligi kuu zipo katika usajili wa dirisha dogo ambalo litafungwa Desemba 15 na siku mbili baadaye mzunguko wa pili wa ligi hiyo utaanza.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic