November 19, 2016Sasa kwa kipindi kirefu Yanga haipo vizuri katika nafasi ya kiungo mkabaji, tunaweza kusema tangu kuondoka kwa Athuman Idd ‘Chuji’ na Frank Domayo, hajapatikana mbadala wao.

Yanga imepiga hesabu baada ya kumtazama kiungo Kenny Ally wa Mbeya City katika mechi mbili dhidi yao na ile dhidi ya Simba na kujiridhisha kwamba anafaa kuwemo kwenye kikosi chao.

Msimu uliopita Yanga ilimsajili Thabani Kamusoko kutoka FC Platinum ya Zimbabwe ili acheza kama kiungo mkabaji, hata hivyo Kamusoko raia wa Zimbabwe ameonekana anamudu zaidi kucheza kama kiungo mshambuliaji.

Hesabu za Yanga wakati huu zimelala kwa Kenny ambaye katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City, Novemba 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Yanga ilifungwa mabao 2-1.

Mabao ya Mbeya City yalifungwa na Hassan Mwasapili dakika ya sita na Kenny akafunga la pili dakika ya 39 huku Donald Ngoma akiifungia Yanga bao pekee dakika ya 45.

Yanga imeona Kenny anaweza kuwasaidia katika kiungo cha ukabaji na tayari baadhi ya viongozi wake wa Kamati ya Mashindano wameanza harakati za siri kuhakikisha wanamsajili mchezaji huyo.

Kidogo Yanga inaweza kukumbana na ugumu kwani Kenny mkataba wake na Mbeya City umebakisha miezi mitatu kumalizika lakini hilo halijawazuia kuzungumza naye kutazama uwezekano wa kumsajili.

 “Ni kweli kabisa tunamtaka Ally kwani tumeona kuwa anaweza kutusaidia katika nafasi ya kiungo mkabaji ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitutesa, tupo katika mazungumzo naye na mambo yakienda vizuri tutamsajili,” alisema kiongozi mmoja wa Kamati ya Usajili ya Yanga.
Pia Yanga imehusishwa na harakati za kumtaka kiungo mshambuliaji wa Mbeya City, Raphael Alpha ili kukiongezea nguvu kikosi chao.

Gazeti hili lilipowasiliana na Kenny alisema: “Taarifa hizo na mimi nazisikia ila kama kweli wananitaka basi wafuate tu utaratibu, tukikubaliana mimi nipo tayari kujiunga nao.”

Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe hakupokea simu yake lakini ofisa habari wa timu hiyo, Dismas Ten, yeye alisema: “Taarifa hizo tunazo mezani kwetu, tumesikia kuwa Yanga wanamtaka Kenny Ally pamoja na Raphael Alpha, kwa upande wetu sisi hatuna tatizo ila tunawaomba wafuate utaratibu tu wa usajili.”

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit ili naye aweze kulizungumzia suala hilo alisema: “Taratibu zote za usajili ni siri ya klabu, hivyo kama kuna mchezaji tutamsajili basi tutawajulisha.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV