Simba SC imeonekana kupania kuuzuia ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu usiende Yanga, ni baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph Omog, kuongeza programu za mazoezi.
Timu hiyo Jumanne iliyopita iliingia kambini mkoani Morogoro kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara uliopangwa kuanza Desemba 17, mwaka huu.
Simba hivi sasa inaongoza kwenye msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 35, ikifuatiwa na Yanga wenye 33 huku Azam FC wakiwa na 25.
Meneja wa timu hiyo, Mussa Mgosi, alisema mikakati watakayoanza nayo kwenye mzunguko wa pili wa ligi kuu ni kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi kuu.
Aliongeza kuwa, watakachokifanya hivi sasa ni kutokubali kuwapisha Yanga wakae juu yao na ndiyo sababu ya kocha kwa kushirikiana na benchi zima la ufundi kukubaliana kuongeza programu za mazoezi kwa asubuhi kufanya mazoezi ya fiziki na jioni ya kimbinu.
“Kiukweli kasi hii ya wapinzani wetu Yanga waliyomaliza nayo kwenye mzunguko wa kwanza ni kubwa, hivyo tunahitaji kuongeza programu za mazoezi kwa ajili ya kuwa fiti.
“Ndiyo maana tangu tumeingia kambini Morogoro tumekuwa tukifanya mazoezi mara mbili kwa siku kwa maana ya asubuhi kufanya mazoezi ya fiziki na jioni ya kimbinu.
“Kikubwa hatutaki kutoka kileleni kwenye msimamo wa ligi kuu na hiyo ndiyo mikakati yetu tuliyojiwekea na ninaamini tutafanikiwa kwa sababu tukiwaruhusu Yanga wakae juu yetu, presha itaongezeka,” alisema Mgosi.







0 COMMENTS:
Post a Comment